19 January 2012

Twiga Stars yanogewa kukaa jeshini

Na Zahoro Mlanzi

TIMU ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), inatarajia kuingia kambini leo
kwenye kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) zilizopo Mlandizi, Pwani baada ya kukoshwa na maeneo ya huko.
Twiga Stars iliweka kambi ya siku zaidi ya 10, Mlandizi kabla haijasafiri kwenda Namibia kucheza na timu ya taifa ya Wanawake ya nchi hiyo, katika mechi ya awali ya mchujo wa kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (AWC).
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema timu hiyo itaanza kambi leo JKT Ruvu, Mlandizi baada ya kupendekezwa hivyo.
"Baada ya kufanya kikao na Benchi la Ufundi la timu hiyo, wameamua kambi iendelee kuwepo huko huko na hii imeamuliwa na wachezaji wenyewe, baada ya kuvutiwa na mazingira ya utulivu ya huko," alisema Wambura.
Alisema timu hiyo itaendelea kujifua katika kambi hiyo mpaka siku tatu kabla ya mechi, ambapo watahamia jijini na watakuwa wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salam ili kuzoea zaidi mazingira ya uwanja.
Wambura alisema jambo hilo litawasaidia, kwani hata kanuni zinashauri kwamba ni vizuri kufanya mazoezi katika uwanja ambao utachezewa mechi na si kuja kuuzoea wakati kwa kuuutumia.
Twiga itarudiana tena na Namibia Januari 29, mwaka huu ambapo mshindi atacheza na Misri au Ethiopia ambapo katika mechi ya awali Misri iliifunga Ethiopia 4-2.

No comments:

Post a Comment