19 January 2012

Cirkovic ashusha presha Simba

Na Zahoro Mlanzi

KOCHA Mkuu wa timu ya Simba, Milovan Cirkovic anaonekana sasa kushusha presha
za mashabiki wengi wa Simba ambao walikuwa na kiu ya kujua kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Kocha huyo tangu atue nchini mwishoni mwa mwaka jana, amekuwa na kazi ya kujua aina ya wachezaji aliokuwa nao pamoja na kutafuta kikosi cha kwanza ili ajipange kuhakikisha wanafanya vizuri katika mashindano mbalimbali.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi wa timu hiyo, Ibrahim Masoud 'Maestro', alisema timu yao inaendelea vizuri na mazoezi na kwamba kocha kwa sasa ameshapata kikosi chake cha kwanza.
"Timu ipo kambini Bamba Beach nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam lakini mazoezi tunafanyia viwanja vya Sigara kila siku na kwamba ipo katika morali nzuri na wachezaji wanafanya mazoezi kwa bidii," alisema Maestro.
Alisema kocha kwa sasa anamalizia kufundisha jinsi timu itakavyocheza baada ya kupatikana kwa kikosi cha kwanza na kwamba anawaomba mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na wasiwasi na timu yao.
Alisema mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwa kiasi kikubwa yamechangia kumrahisishia kocha huyo kutafuta kikosi cha kwanza kwani wachezaji kila mmoja alicheza katika kiwango cha juu ili kumshawishi kocha ampe nafasi.
Alisema mbali na mashindano hayo, pia mechi za kirafiki walizocheza baada ya kumalizika kwa mashindano hayo, zilimsaidia kocha huyo kupata timu anayoihitaji.
Simba inajiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara ambapo watashuka uwanjani Jumatano kwa kuumana na Coastal Union ya Tanga pamoja na Kombe la Shirikisho ambapo watacheza na Kiyovu ya Rwanda.

No comments:

Post a Comment