16 January 2012

PST yamsimamisha Agapeter

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Masumbwi Tanzania (PST), limemsimamisha Makamu wa Rais wa shirikisho hilo, Agapeter Mnazareth kutokana na kudaiwa kufanikisha pambano lisilo la ubingwa kati ya Karama Nyilawila na Fransic Cheka.

Pambano hilo limesababisha Nyilawila kuvuliwa ubingwa wa Dunia wa WBF baada ya kutakiwa asipigane pambalo lake dhidi ya Cheka mpaka atakapomaliza pambano lake ya kutetea ubingwa huo.

Lakini bondia huyo alikataa kusimamisha pambano hilo kwa madai anachoangalia kwa sasa ni pesa na mambo mengine yatafuata.

Kwa mujibu wa barua ambayo gazeti hili iliinasa kutoka PST kwenda kwa Agapeter Dar es Salaam jana na kusainiwa na Rais wa shirikisho hilo, Emmanuel Mlundwa ilieleza kwamba wamefanya hivyo kutokana na shirikisho hilo kutotaka kuhusika na upoteaji wa heshima ya nchi.

“Pambano hilo la Nyilawila na Cheka lilisababisha mpaka Nyilawila kujivua ubingwa, ambao ulikuwa na heshima kubwa ambao ndio umeipa kibali PST kufanya kazi nchini,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.

Ilieleza kutokana na hilo, wameamua kumsimamisha Agapeter tangu Januari 13, mwaka huu ili kuchunguza kuhusika kwa upoteaji wa heshima la taifa hilo.

Iliongeza katika muda ambao wamemsimamisha, kiongozi huyo anaweza kuendelea na shughuli zake za masumbwi na vyama vingine vya ndondi hapa nchini.

Alipotafutwa kiongozi huyo kupitia simu yake ya kiganjani, aliita bila kupokelewa na baadaye ilikatwa.

No comments:

Post a Comment