13 January 2012

Na Rehema Mohamed

WANAFUNZI wanne kati ya 50 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wanaokabiliwa na kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ya kudaiwa kujihusisha na fujo chuoni hapo wamekosa dhamana baada uongozi wa chuo hicho kujivua kuwadhamini.

Wanafunzi hao ni Bw.Elias Mwambaja,Bw.Alfonce Lusako,Bw.Moris Devis na Bw.Jabiri Ndimbo na wamerudishwa rumande.

Wanafunzi hao walikosa dhamana jana mbele ya Hakimu Bi.Waliarwande Lema,wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Ilidaiwa kuwa uongozi wa chuo ulijitoa kuwadhamini wanafunzi hao baada ya kubainika kuwa mmoja wao Bw.Said John (31) ambaye jina lake halisi Bw.Hassan Selemani sio mwanafunzi wa chuo hicho na ana kesi ya unyang'anyi wa kutumia silaha katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 23 itakapokuja kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali.

Katika kesi hiyo wanafunzi hao pia wanakabiliwa na kosa la kufanya mkusanyiko usio kuwa wa halali na kusababisha uvunjifu wa amani eneo la chuoni hapo.

Shitaka lingine ni kufanya mkusanyiko usio wa halali kwa lengo la kufanya mgomo baada ya kutolewa amri na jeshi la polisi la kutaka watawanyike eneo hilo.

1 comment:

  1. Enyi wanafunzi wa chuo kikuu,mnaona wenzenu wanavyotaabika.Kwa nini hamtaki kutumia njia za kistaarabu kutatua matatizo?.Hiyo ni hasara kubwa kwenu,wazazi wenu na taifa kwa ujumla.

    ReplyDelete