18 January 2012

Mtema aagwa Dar,

wabunge 50 kuongoza mazishi yake

Na Peter Mwenda

MAKAMU wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal na Wwaziri Mkuu Bw. Mizengo Pinda, jana waliongoza mamia ya wananchi
, viongozi wa Serikali na vyama vya siasa kuuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bi. Regia Mtema (31), aliyefariki kwa ajili ya gari.
Akitoa salama za Serikali kwa familia, wabunge, ndugu, jamaa na marafiki, kabla mwili huo haujasafirishwa kwenda Ifakara, mkoani Morogoro kwa mazishi yaliyopangwa kufanyika leo, Bw. Pinda alisema Bi. Mtema, alikuwa mtu mwenye karama ya pekee maishani mwake.
Alisema enzi ya uhai wake, Bi. Mtema alikuwa na uwezo mkubwa wa kufikiri na kutoa hoja zenye lengo la kujenga.
CHADEMA itaziba pengo la Mtema, lakini hawatampata mtu mwenye karama kama yeye, pale alipokosolewa alikuwa akiomba radhi,¡± alisema Bw. Pinda na kuongeza kuwa, yeye atamkumbuka Bi. Mtema kutokana na uwezo wake ndani ya bunge.
Kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni na Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe, alisema alimfahamu Bi. Mtema alipotembelea Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Machame, iliyopo mkoani Kilimanjaro mwaka 2001, yeye akiwa Mbunge wa Hai.
Bi. Mtema ndiye alisoma risala kwa niaba na wanafunzi wenzake,
alitoa mawazo ya kupenda mageuzi nchini na alipokuwa mwanafuzi wa Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA), alijiunga na CHADEMA,¡± alisema Bw. Mbowe.
Aliongeza kuwa, katika uhai wake Bi. Mtema alikuwa mmoja wa vijana waliopata mafunzo ya kuwa viongozi wa chama pamoja na Mbunge wa Ubungo, Bw.  John Mnyika (Bunge wa Ubungo) na Bw. John Mrema.
Alisema marehemu hakufurahishwa kupangiwa majukumu mepesi kutokana na ulemavu wake bali alitaka afanye kazi kama wengine wasio na ulemavu wowote.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda alisema Bi. Mtema alipata ujasiri wa kuingia kwenye siasa baada ya kushiriki semina mbalimbali alizokuwa akizitoa kama mkufunzi kabla hajachaguliwa kuwa Spika wa Bunge.
Alisema ujasiri huo ndiyo ulimfanya Bi. Regia kuingia katika kinyang'anyiro cha uchaguzi mkuu mwaka 2010 kupitia chama chake na kushika nafasi ya pili baada kupata kura 38,000 ambazo ni asilimia 41.
Wabunge 50 wameondoka jana na mwili wa marehemu kwenda Ifakara ili kushiriki mazishi.
Mwandishi Wetu Rabia Bakari anaripoti kuwa, Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), limetoa salama za rambirambi kutokana na kifo cha mbunge huyo.
Mwenyekiti wa shirikisho hilo, Bi. Lupi Maswanya, alisema  wameshitushwa na kifo hicho ambacho kilitokea Januari 14 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment