18 January 2012

Sakata la Posho:

Bunge lachongea
mihimili mingine

Ndugai asema watumishi wake wanalipwa zaidi ya wabunge
Awavaa viongozi wa dini, adai posho wanazolipwa ni kubwa
Azungumzia sakala la Hamad Rashid, David Kafulila, Jairo

Na Waandishi Wetu
SAKATA la nyongoza ya posho za wabunge kutoka sh. 70,000 hadi 200,000, limechukua sura mpya
baada ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Bw. Job Ndugai, kutaka posho za watumishi wa mihimili mingine ya dola, zihojiwe na kuwekwa wazi ili zijulikane.
Bw. Ndugai aliyasema hayo juzi usiku katika mahojiano maalumu ya kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na televisheni ya ITV.
Alisema wananchi wana haki ya kulalamika juu ya nyongeza hiyo kwa sababu hawajui viwango vya posho vilivyopo mahakamani, serikalini na posho za wastaafu.
Kinachochangia malalamiko katika sakata hili ni kutokana na uwazi uliowekwa tofauti na ilivyo katika mihimili mingine, kama wangekuwa na uwazi katika posho zao na maslahi mengine wanayolipwa, hizi za wabunge zisingepigiwa kelele.
Nyongeza ya posho za wabunge ni ndogo sana ndio maana nasema kama kungekuwa na uwazi, wangeacha hizi za wabunge na kupigia kelele posho za mihimili mingine,¡± alisema Bw. Ndugai.
Aliongeza kuwa, mshahara wa mbunge ni sawa na ule anaolipwa ofisa wa kawaida wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) na ofisa wa ngazi ya chini bandarini.
Alisema ili kuondoa mkanganyiko huo ni vyema kukawepo tume maalumu kama ilivyo katika nchi nyingine ambayo itaangalia hali ya uchumi wa nchi na kupanga posho kwenye sekta zote bila kuwepo usiri.
Bw. Ndugai alisema posho zitokanazo na kodi za wananchi hazipaswi kuwa siri kuanzia zile wanazopata Wakuu wa Wilaya hadi maofisa wa ngazi za juu.
Alifafanua kuwa, serikalini hakuna posho za aina moja bali kuna tofauti kubwa ingawa watu wengi wanaopinga nyongeza ya posho za wabunge hawashauri wanataka ziweje.
Hata kanisani, wale waliopo juu wanapata posho nyingi kushinda wachungaji wa kawaida lakini kwa sababu hakuna uwazi wananchi hawajui, tutengeneze chombo ambacho kitaangalia na kuweka wazi suala la posho kwa wachungaji, maaskofu na serikalini,¡± alisema.
Kauli ya Bw. Ndugai, ilionekana wazi kuwajibu viongozi wa dini, ambao wamekuwa wakipinga ongezeko la posho akiwemo Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Kardinali Pengo alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa,
viongozi wa Serikali na umma wakiwamo wabunge, wanapaswa kuacha ubinafsi badala yake wafanye kazi kwa kuwafikiria zaidi wananchi.
Sisi Wakristo tunaamini kuwa, Kristo licha ya kutumwa na Mungu Baba kuja kutukomboa wanadamu, alifanyika mwili na kuzaliwa katika hali ya umaskini na ufukara ili atukomboe, viongozi wa Serikali, dini na watumishi wa umma, inatupaswa kuiga mfano huo,¡± alisema Bw. Ndugai.
Aliongeza kuwa, wakati umefika wa kuangalia kama posho ni sawa kulipwa au hapana, kwani zipo nyingi na kila aina hivyo ziangaliwe kupitia chombo kitakachokuwa kimeundwa ili wananchi wafahamu hatua itakayosaidia kuondoa mjadala huo.
Chombo hiki kitafanya tathmini kama wabunge wanastahili kuongezwa posho au la, kama ni kikubwa wanastahili kupata kiasi gani na vipaumbele ni vipi,¡± alisema Bw. Ndugai na kuwataka Watanzania kuwa na imani na viongozi wanaowachagua.
Pia Bw. Ndugai alimgusa kwa mara nyingine Waziri Mkuu mstaafu, Bw. Frederick Sumaye, akisema alizungumza vizuri suala hilo, lakini hakushauri nini kifanyika kwa kuwa amewahi kuwa kiongozi wa juu serikalini.
Hivi karibuni Bw. Sumaye ambaye alihojiwa katika kipindi hicho, alizungumzia suala la posho za wabunge lakini Bw. Ndugai alipinga maelezo yake na kudai kuwa, wakati kiongozi huyo mstaafu akiwa bungeni, aliridhia kupanda kwa posho za wastaafu ili anufaike.
Majibu ya Bw. Ndugai yalipingwa na makundi ya watu mbalimbali wakiwemo wasomi, wanasiasa na viongozi wa dini akiwemo Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye ametishia kulifikisha sakala hilo mahakamani.
Sakata la Kafulila, Hamad Rashid
Akizungumzia kufukuzwa uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi na Bw. Hamad Rashid Mohamed, Jimbo la Wawi, Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Ndugai alisema suala hilo linaanzia kwenye katiba ambayo inasema mtu hawezi kuwa mbunge bila kuwa mwanachama wa chama cha siasa.
Alisema chama kikimwandikia barua spika kuwa kimemvua mbunge wake uanachama, anakuwa amepoteza sifa ya kuwa mwakilishi wa wananchi hivyo kinachotakiwa kufanywa na spika ni kutangaza kuwa hao si wabunge.
Aliongeza kuwa, Ofisi ya Bunge imeshindwa kufanya hivyo kwa sababu suala hilo lipo mahakamani hivyo haiwezi kufanya kitu chochote ambapo katiba mpya inapaswa kuwa na kipengele cha mgombea binafsi kwani wabunge wanachaguliwa na wananchi.
Bw. Ndugai alisema katika kipindi hiki cha mchakato wa Katiba Mpya ni muhimu wananchi wakaangalia kipengele hicho.
Hatima ya Jairo
Akizungumzia hatima ya aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, Bw. David Jairo, Bw. Ndugai alisema majibu ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na bunge, yatawasilishwa kwenye kikao kijacho cha bunge, ambacho kitaanza Januari 31 mwaka huu.
Kila Mtanzania atasikia hatima ya Jairo katika kikao kijacho, lakini mambo yanakwenda vizuri,¡± alisema Bw. Ndugai.
Awataka wananchi kusubiri hatima ya Jairo bungeni

1 comment:

  1. KIINI CHA TATIZO LA MALIPO YA POSHO NA MALIPO MENGINE YANAYOFANYWA NA SERIKALI BILA KUZINGATIA HALI HALISI YA UCHUMI WETU NI NDOA YA UTATU ILYOPO KATI YA MHIMILI WA BUNGE NA SERIKALI (EXECUTIVE POWER) NA MAHAKAMA.

    SERIKALI NDIYO ILIYOPEWA JUKUMU KIKATIBA KUSIMAMIA MATUMIZI NA MAPATO YA NCHI BAADA YA KUPITISHWA NA KUIDHINISHWA NA BUNGE KWENYE BAJETI.

    BUNGE LIKIOMBA NYONGEZA ZA POSHO AU MALIPO MENGINE KAMA YA MIKOPO YA MAGARI YA KIFAHARI SRIKALI INAWAPA. SERIKALI NAYO IKIOMBA KUONGEZEWA POSHO NA MARURURUPU ZAIDI INABIDI MHIMILI WA BUNGE UWAPE KAMA FADHILA ILI KUWAZIBA MDOMO. HII NI NIPE NIKUPE ITAKAYOENDELEA KILA MARA.

    MHIMILI WAMAHAKAMA UNAWAJIBIKA KUTOA UAMUZI KATI YA BUNGE NA SERIKALI ILI KUVUNJA HUU MTINDO WA NIPE NIKUPE LAKINI NAYO MAHAKAMA IMEINGIZWA KWENYE NDOA HII YA UTATU.

    NANI ATOE UAMUZI? ITABIDI WENYE MALI/WENYE HISA AMBAO NI WANAANCHI WA TANZANIA WATOE UAMUZI. BUNGE WALA SERIKALI, HAZITAKI KWENDA MAHAKAMANI KUTAFUTA SULUHU. ITABIDI WANANCHI WAENDE MAHAKAMANI ILI HAKI ITENDEKE.

    ReplyDelete