19 January 2012

Madega aipa 'dawa' Yanga kuiua Zamaleki

Na Zahoro Mlanzi

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Iman Madega ameitaka timu hiyo kufanya maandalizi ya nguvu kabla haijacheza na Zamaleki
huku wachezaji watambue umuhimu wa mechi hiyo kwa kusahau matatizo waliyokuwa nayo.
Mbali na hilo, amewataka wanachama na wadau wa timu hiyo kuwa na umoja na mshikamano hususani katika kipindi hiki cha maandalizi ya kujiandaa na mechi hiyo, kwani tofauti zao zitatoa mwanya kwa wabaya wao kuwaingia.
Yanga na Zamaleki zinatarajiwa kukutana kati ya Februari 16, 17 au 18 mwaka huu Dar es Salaam katika mechi ya awali ya Klabu Bingwa Afrika.
Akizungumza Dar es Salam jana, Madega alisema Zamaleki ni timu kubwa Afrika na imewekeza katika soka, hivyo wachezaji wa Yanga wanapaswa kutambua wanacheza na timu ya aina gani.
"Tunajua timu zetu zina matatizo mengi lakini katika mechi kama hii tena unacheza na timu maarufu Afrika, hawana budi kuweka mbali matatizo waliyonayo na kutilia mkazo katika mchezo huo," alisema Madega na kuongeza;
"Nilisikia kuna wakati wachezaji hawakupata mishahara lakini hilo ni jambo la kawaida, kikubwa ni kufunga mkanda na kwenda mbele kwani ikifanikiwa kuvuka hatua hiyo, sina shaka sifa watakayopata ni kubwa sana," alisema.
Alisema kipindi kilichobaki kabla ya kucheza mechi hiyo ni kikubwa kwa maandalizi katika nafasi wanazoona zimepwaya kufanya marekebisho kwani kama si kujipanga sasa muda nao utazidi kwenda.
Alisema Yanga ni moja ya timu zinazoiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa, hivyo ni wajibu wa serikali kutia mkono kipindi hiki cha maandalizi na si kujitokeza baada ya timu kufanya vizuri na kutoa pongezi nyingi.
"Tumezoea kuona baadhi ya wabunge, wafanyabiashara wanajitokeza baada ya kuona timu imefanya vizuri, mimi naomba wadau wote wa soka hususani wa Yanga kujitokeza wakati huu wa maandalizi," alisema Madega.
Alisema si serikali pekee hata TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu), wana nafasi ya kutoa msaada katika hilo kwa kuangalia wapi wanaona Yanga haijaweka sawa mambo yao na kutoa mchango wao.
Madega aliongeza, pia Yanga inatakiwa itambue ikicheza vibaya kuna baadhi ya mashabiki wa Simba huzomea lakini watakapoonesha soka safi la kueleweka ana imani wanaozomea sasa wataishangilia.

No comments:

Post a Comment