19 January 2012

African Lyon yaipa TFF siku 30

Na Amina Athumani

KLABU ya soka ya African Lyon, imelipa siku 30 Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
, kukaa nao meza moja kuzungumzia matatizo yao na kama itashindikana watajitoa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa African Lyon, Sherally Hammed alisema klabu yake imekuwa na matatizo mengi ambayo chanzo chake ni TFF, hivyo wanawapa siku 30 ili kukaa pamoja na kufikia makubaliano.
Alisema wao kwa nguvu zote wanaelewa kuwa TFF, ina mpango madhubuti wa kuishusha timu hiyo daraja ama kuiondoa katika ramani ya soka.
Hammed alisema wamefikia kuipa TFF siku 30 ni kutokana na fedha za Vodacom za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, kwani wao walipokea sh. milioni 3.5 pekee wakati klabu nyingine zimepata zaidi ya hizo.
Pia Msamaji huyo aliilalamikia ratiba ya Ligi Kuu, ambapo alisema timu zote ambazo zimekuwa zikienda kucheza mechi Kanda ya Ziwa, zimekuwa zikicheza mechi zote mbili ya Toto FC na Kagera Sugar, lakini wao Lyon hawajawahi kukutana nacho.
"Kama hiyo haitoshi mechi yetu ya mwisho wametupeleka Manungu, Turiani kucheza dhidi ya JKT Ruvu na hali sisi na JKT, uwanja wetu ni Chamazi halafu wenyeji wa Turiani Mtibwa Sugar, wamewapeleka Morogoro kucheza dhidi ya Moro United ni vigezo vipi vilivyowekwa kutupeleka sisi na si Simba wala Yanga?," alihoji Hammed.
Alisema pamoja na hayo wanaidai TFF sh. milioni 35, za tiketi ambazo shirikisho hilo liliwaomba wazichape Marekani mwaka 2009, ambazo thamani yake ni sh. milioni 40.
Msamaji huyo alisema katika fedha hizo, TFF imelipa sh. milioni 5 pekee, tangu wakati huo.
Alisema tiketi hizo zilitumiwa kwa mechi mbalimbali, zikiwemo za Taifa Cup na Kagame Cap.
"Nathubutu kusema kuwa TFF  haipo makini kwa jambo lolote kutokana na kwamba wakati sisi tunainunua timu ya Lyon mwaka 2009/2010 timu hii ilipata zawadi ya sh. milioni 5 kama timu yenye nidhamu,"alisema na kuongeza kuwa.
"Cha kushangaza Kaimu Katibu MKuu Sundey Kayuni aliandika hundi kwa jina la Kasim Dewji huku ikijua fika kuwa sisi ndio tunaomiliki timu na hata kama yeye ndiye aliyekuwa akimiliki timu bado jina lingebaki la timu na si la mtu binafsi,"alisema Hammed.
Alisema kutokana na suala hilo kuna uwezekano mkubwa wa fedha hizo wakagawana  viongozi wa juu na ndio sababu ya TFF kulikingia kifua na kwamba wanachodai wao ni kurejeshwa kwa pesa hizo kwa kuwa ni mali ya wachezaji.
Katika hatua nyingene klabu hiyo ya Lyon imelaani kitendo cha aliyekuwa mchezaji wa klabu hiyo Yusufu Soka kukamatwa nchini Sweden kutokana na kukumbwa na kashfa ya dawa za kulevya na kwamba wanaomba vyombo dola viingilie kati na sheria ichukue mkono wake.
Alisema TFF Kupitia Kaimu Katibu Mkuu Kayuni na wakala waliamua kumpeleka mchezaji huyo Sweden kwa ajili ya kufanya majaribio na kwamba vielelezo vya mchezaji huyo alivyoondoka na wahusika wa safari hiyo vipo katika klabu hiyo.

No comments:

Post a Comment