23 December 2011

Yanga yahifadhi waathirika 400

Na Zahoro Mlanzi

MVUA kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam na kusababisha mafuriko yaliyoleta maafa makubwa, zimesababisha Klabu ya
Yanga, kutoa hifadhi kwa waathirika 408 kukaa Makao Makuu ya timu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani, jijini.

Mvua hizo zilianza kunyesha usiku wa kuamkia Jumanne ambapo mpaka juzi usiku, watu 13 waliripotiwa kufariki na wengine wakikosa makazi ya kuishi kutokana na mvua hizo kuingia katika nyumba zao.

Akizungumza na gazeti hili Makao Makuu ya klabu Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema idadi ya watu walioathirika na mvua hizo inazidi kuongezeka ambapo wameona ni bora watoe huduma ya makazi klabuni kwao.

"Hali hapa klabuni kwetu ni mbaya sana, uwanja umejaa maji pamoja na ukuta wa upande mmoja umeanguka, lakini kibaya zaidi wakazi wengi wa maeneo ya hapa wamekosa hifadhi, kama klabu tumechukua jukumu la kuwahifadhi waathirika hao.

"Jana (juzi), tuliopkea waathirika 200 na kuwapa makazi hapa klabuni, lakini kadri muda unavyosonga mbele tunazidi kuchukua watu zaidi ambapo mpaka sasa (jana mchana), tuna waathirika 408 hapa klabuni kwetu," alisema.

Mbali na hilo, pia alizungumzia maandalizi yao ya mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya ESCOM ambapo alisema, timu hiyo itatua nchini kati ya Ijumaa au Jumamosi kwa ajili ya mechi itakayopigwa Jumatatu.

Wakati huohuo, Sendeu alizungumzia hali ya kiungo wao, Athuman Idd 'Chuji', ambaye aliumia katika mechi ya kirafiki dhidi ya Azam, ambapo alisema alipata mshtuko katika kifundo cha mguu lakini hivi sasa anaendelea vizuri.

No comments:

Post a Comment