23 December 2011

Ujerumani yaandaa filamu ya Kitanzania

Na Gabriel Moses

KITUO cha Utamaduni cha Ujerumani kilichopo Upanga jijini Dar es Salaam, kimeandaa filamu inayoelezea historia ya Mtanzania wa kwanza kuigiza na Wajerumani, kabla na baada ya
Tanzania kupata uhuru.

Filamu hiyo inakadiriwa kutumia zaidi ya sh. milioni 70, ambayo itayashirikisha maeneo muhimu ya historia ya Tanzania na mengine kutoka nchini Ujerumani.

Akizungumza Dar es Salaam jana, MKurugenzi wa Utamaduni wa Ujerumani, Eleonare Sylla alisema filamu hiyo inaandaliwa kwa ushirikiano wa pamoja, kati ya Tanzania na Ujerumani katika kuonesha mabadiliko yaliyopo kabla na baada ya uhuru.

Eleonare alisema Wajerumani, wamekuwa wakihamasika kutaka kufahamu historia ya Mtanzania wa kwanza Bayume Mohamed Hussein, aliyezaliwa mwaka 1904 kufanya filamu akiwa na Wajerumani nchini humo.

Alisema Hussein amekuwa kivutio kikubwa kwa Wajerumani, ndipo hamasa ya kutaka kufahamu chimbuko lake liliibuka na kuamua kufanya filamu hiyo itakayorekodiwa katika maeneo mbalimbali ya kihistoria hapa nchini na kisha kuhaririwa nchini Ujerumani.

Kwa mujibu wa MKurugenzi huyo zaidi ya sh. milioni 70, zitatumika katika uandaaji wa filamu hiyo ikijumlisha gharama za malazi, kulipia maeneo ya kihistoria na mengineo.

Alisema filamu hiyo pia inawashirikisha Watanzania wawili, ambao ni watayarishaji wa filamu David Kyungu na Rashid Faraji, wengine ni raia wa Ujerumani ambao ni Eva Knopf, Rainer Hoffmann na Nadja Hermann.

Jina la filamu hiyo litajulika kwa jina la Mohamed Hussein, kutokana na Wajerumani wengi kuguswa na historia yake akiwa Mwafrika wa kwanza kufanya filamu nchini humo.

Hussein alikwenda nchini Ujerumani enzi za utawala wa Wajerumani, akiwa na umri wa miaka tisa.

No comments:

Post a Comment