22 December 2011

Waziri Simba awataka maofisa kubuni miradi

Na Ramadhan Libenanga,
Morogoro

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto Bi.Sofia Simba amewataka maofisa Maendeleo ya Jamii  ngazi zote kuhakikisha wanatekeleza na kubuni  miradi mbalimbali inayopelekwa katika maeneo yao kwa ajili ya kusaidia jamii hususani makundi maalumu.

Waziri Simba aliyasema hayo jana Mjini Morogoro wakati alipokuwa akifungua  Mkutano Mkuu wa mwaka wa sekta ya maendeleo ya jamii, mkutano uliowahusisha maofisa mendeleo ya jamii wa halmashauri, mikoa, wakuu wa vyuo vya maendeleo ya jamii,ambapo alisema kuwa  sekta ya maendeleo  ya jamii ina jukumu la kuwaandaa wananchi katika
kutekeleza miradi.

Alisema kuwa wizara hiyo pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali lakini kuna haja ya kutafuta mitazamo na kupanga mikakati ya kuendana na wakati ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa wanawake hususani katika vikundi vya VIKOBA  ambavyo vimeonekana kufanya vizuri katika marejesho.


“Kinachotakiwa hapa ni kuondokana na dhana za kale tuendane na utandawazi wa kimtandao,,tutoe huduma kwa njia za kisasa zaidi,ninyi maofisa ustawi ndio tegemeo kwa Taifa letu,”alisema Waziri Simba

Aliwataka wakuu wa vyuo vya maendeleo ya jamii FDC kuhakikisha wanafikiria  namna ya kuongeza wanafunzi katika vyuo kwa kufikiria miradi ya kuinua vyuo vyao ikiwa ni pamoja na kuhamasisha jamii kujiunga na  FDC.

Waziri huyo alitolea mfano kwa Chuo cha Maendeleo ya Jamii (FDC) Wilaya Nzega mkoani Shinyanga ambacho alikitembelea na kukuta majengo mazuri lakini  ambayo hayana wanafunzi kutokana na walimu na uhamasishaji wa kutosha wa wanafunzi kujiunga katika chuo hicho.


Alisema kuwa FDC nyingi nchini ziko katika hali mbaya na bado zimeonekana kuwa mifumo ya kizamani ambayo kwa sasa imepitwa na wakati hivyo  kuwaangiza wakuu hao kuhakikisha na wanabadili mifumo yao.

No comments:

Post a Comment