02 December 2011

Walimu kugoma

*Wasema wamechoka kunyanyaswa na serikali
*Walaani posho za wabunge, wadai huo ni usaliti
*Wasisitiza maadhimisho uhuru hayana tija kwao


Na Anneth Kagenda

WAKATI joto la mchakato wa Katiba Mpya likiendelea kutikisa nchi, Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimetangaza mgomo isio na kikomo wa
kutoingia darasani ifikapo Januari 2012 hadi Serikali itakapolipa madeni yote ya walimu ya sh. bilioni 49.6.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Rais wa chama hicho Bw. Gratian Mukoba, alisema wamechoshwa na unyanyasaji unaofanywa na Serikali pamoja na kushindwa kuwalipa fedha zao kwa muda mrefu sasa.

“Ndugu zangu waandishi, baada ya kupitia na kuhakiki madai ya walimu, CWT tulipeleka serikalini madai ya walimu tangu Juni mwaka huu, pia tumefanya vikao kadhaa na Serikali na hatimaye ikakubali kutatua kero hizo Novemba na Desemba mwaka huu.

“Kwa kuwa Novemba umeisha, Serikali haijasema lolote kuhusu madai haya, CWT tunafahamu kuwa Serikali inaona mgomo wa walimu wakati huu hauna madhara kwa sababu wanafunzi wamemaliza mitihani na shule zinaelekea kufungwa lakini ukweli ni kwamba, hakuna mgomo usio na madhara,” alisema.


Alisema kwa kuwa Serikali imeshindwa kuheshimu makubaliano yao, shule zikifunguliwa Januari 2012, walimu tutaendelea kuwa likizo hadi kero zao zitakapotatuliwa.

Alitaja baadhi ya kero za walimu kuwa ni kulipwa madeni yao yaliyohakikiwa sh. bilioni 49.6, pamoja na kufutwa kwa waraka kandamizi unaowarudisha nyuma walimu walio jiendeleza kielimu.

Alisema wapo walimu waliojiendeleza kielimu lakini bado hawajapandishwa madaraja, kuongezwa mishahara na stahili nyingine kutokana na waraka huo.

“Kufutwa kwa waraka huu, itakuwa suluhisho la mgogoro kati yetu na Serikali kama mwajiri, kero nyingine ni baadhi ya walimu kutolewa katika mfumo wa ulipaji mishahara, walimu kukatwa mapato yao kinyume na taratibu, baadhi yao kutoongezwa mishahara kwa wakati na madai ya posho za kusimamia mitihani mbalimbali,” alisema Bw. Mukoba.

Alitoa wito kwa walimu wote kuwa na mshikamano kwa kuonesha ushirikiano wa hali ya juu katika kutekeleza maamuzi hayo muda utakapofika ili waweze kuvuka salama na kuwataka wazazi  kuwaelewa na kuungana nao katika kudai haki zao ili watoto wao wapate elimu bora.

“Mtakubaliana nami kuwa kila mmoja wetu ni shahidi wa kero zinazowakumba walimu, lazima zifikie mwisho ili baadaye walimu wafanye shughuli zao katika mazingira mazuri na kuacha kunyanyaswa,” alisema.

Akizungumia maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Bw. Mukoba alisema CWT haioni sababu ya sherehe hizo wakati madai ya walimu yanaendana na miaka hiyo.

“Fedha nyingi inapotea katika maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru, lakini watoto wanasoma shule tangu asubuhi hadi mchana wakiwa na njaa, hakuna vitabu vya kutosha, madarasa mabovu na hakuna vifaa vya kufundishia, sasa tunasherekea kitu gani au ili iweje,” alihoji Bw. Mukoba.

Akizungumzia posho za wabunge, Bw. Mukoba aliweka wazi kuwa inasikitisha kuona wakati walimu wengi hawapati sh. 200,000 baada ya makato, mbunge analipwa sh. 330,000 kwa siku jambo ambalo alilifananisha na wawakilishi hao kuwaibia Watanzania.

“Wabunge waache wizi, huu ni usaliti na dharau, nasema hivi kwa sababu hawaoni hata aibu kusaini posho nyingi wanapokuwa katika vikao vya Bunge wakati walimu wanalala kwenye nyumba mbovu na kunyeshewa mvua.

“Idadi ya wabunge ni 357, wanapokuwa kwenye vikao na kusaini posho hizi kila mmoja, malipo hayo yanafikia sh. milioni 117.8, ukizigawa unapata milioni tisa sawa na nyumba 13 za walimu, kwa siku 10 utapata nyumba 130, hamuoni kwamba huu ni usaliti wa hali ya juu,” alihoji.

Akitoa takwimu za makato ya walimu, Bw. Mukoba alisema wanakatwa sh. 5,000 na 3,000, michango maalumu sh. 2,000, Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) sh. 16,285 na Michango ya CWT sh. 6,514.

Alitaja michango mengine kuwa ni kodi sh. 25,330.06, michango ya kuendeshea akaunti katiba benki, sh. 46,654, Mwenge wa Uhuru sh. 500, Bima ya Afya sh. 9,771 na kufafanua kuwa jumla ya fedha anazokatwa hadi kufikia Oktoba 31 mwaka huu, itakuwa ni sh. 210,645,94.

21 comments:

  1. Hakuna taifa liwezalo kuendelea bila rasilimali watu. Na hao hutokana na waalimu. Sasa iweje waalimu nchini kwetu wateseke vile? Huyo mtoto wa mkulima halioni hili?Angalao Lowassa angeweza kufanya kitu lakini si huyu anayeangua kilio kwa ajili ya albino kuuawa badala ya kuchukua hatua za kukomesha. You have our support teachers; move on.

    ReplyDelete
  2. Waalimu, hamtambui kuwa mkigoma:

    1. Mtajiumiza wenyewe na familia zenu kwa kuwa maisha ni magumu,kipato kidogo. baadhi mnayo mikopo n.k. Je mtamuduje maisha wakati wa kipindi cha mgomo?

    2. Watoto wenu na wa Watanzania wataumia kwa kuwa kosa ambalo sio la kwao?

    Kutatua matatizo yenu, nashauri mfanye uamuzi wa dhati wa kutumia silaha yenu kubwa ya demokrasia yaani KURA zenu kuwaondoa madarakani wale viongozi mnaosema wanawadanganya, hawasikilizi n.k. Kama wengine mtakaowachagua watafanya hivyo hivyo, mtumie silaha hiyo kuwaondoa. Unganeni na wananchi wote wenye kujali shida zenu. Haisaidii kwenda mabarabarani kuandamana au kukaa nyumbani. Viongozzi wanaogopa sana hii silaha ya KURA!

    ReplyDelete
  3. me nasema wagome hata mwezi,hata wakifundisha wanachopata ni hasi tupu.na vikao vya bunge vikianza wagome pia.watoto wa wakubwa hawasomi hizo shule wanazogoma waalimu kwa hiyo hawaguswi.siye wa chini ndo tunaguswa;ndo maana hawalipwi,ngoja st marys na shule za bei mbaya wagome wabunge watawafata wenye shule ili walimu wao walipwe wafundishe watoto wao.wanagoma wanafundisha watoto wa mkulima nani atajali,kwani anasoma wake?walimu wamesahaulika,wamedharauliwa,wamedhalilishwa,hawana tena thaman,fikiri hata pesa ya uchaguzi wanawapunja,wamepunguziwa utu sana,hata me nakasirika kwa hilo.wagome tuone watawapa pipi gani msimu huu.

    ReplyDelete
  4. naungana na 12:44, me nasema wagome tu, mpaka kieleweke, ni kweli mbona wabunge hawagomi,si wanalipwa vizuri?wagome wakati wa kikao cha bunge ili bunge lipate cha kujadili,maana katiba inaishia hiyo.wajadl hoja ya waalimu basi.na walipwe msimu wa bunge la sivyo na wabunge wagome!Yes.

    ReplyDelete
  5. Matatizo ya walimu niyamuda mrefu sana na kwa sababu serikali ya Tanzani hawajali waamu kuongezeana posho badala ya kusaidia raia wake.Hivi kweli tuna viongozi wanaoweza kufikiria mambo ya maana badala ya matumbo yao?

    ReplyDelete
  6. huyu mchangiaje anayemuingiza lowasa hapo juu asituchefue.ajenge hoja lowasa amefanya nini kipindi chote alichokuwa kiongozi zaidi ya kututengenezea matatizo yanayotusumbua mpaka sasa (yaani kutuingiza kwenye mikataba ya kampuni za mfukoni kama richmond)tuache kampeini za kuweka watu wanaoteketeza nchi.
    anzia alopokuwa ardhi kazi ilikuwa rushwa kuna madudu aliyafanya huko hata leo hayarekebishiki huyu ni mharibifu kupita kiasi.vyote alivyofanya sioni kilicho endelevu.watanzania tuogope ujasili wa kitapeli maana kiuhalisia hakuna mwizi au jambazi asiye jasili na tukitaka ili mradi ujasili basi tutawapa majambazi madaraka.tutafute jasili aliye timamu na anayefuata utaratibu katika kutawala nchi mfano kuna watu kama magufuli ni moja ya mifano hai.na tuogope majasili wa kufanya mambo kwa faida zao. kumbukeni mwalimu nyerere alivyomwambia lowasa wakati alipoingiza jina lake katika kinyang'anyiro cha mwaka 1995.

    ReplyDelete
  7. mambo ya kina lowassa achana nayo,wale ni matajiri a kimataifa,tunataka haki za waalimu zifikie muafaka.migomo ni kufikisha ujumbe,ndo maana akachangia mtu kuwa tena wagome wakati wa bunge.nasubiri hilo gomo.kama nao watagoma huko bungeni tuone.kama wanapenda haki za waalim nao wabunge wagome tuone kama waalimu hawatalipwa.wagome kuingia bungeni kama wana uchungu na waalimu waliowafundisha wao na watoto wao.tusubiri

    ReplyDelete
  8. Tatizo kubwa ni kuwa UCHUMI wetu unatumika SIASA, hivyo nchi haitaendelea hata siku moja, itabaki kudanganyana tu. Ili NCHI yoyote iendelee SAISA inatakiwa kutumikia UCHUMI na si vinginevyo. Leo mtaalamu aliyehangaika kusoma miaka mingi na kufanyakazi nzito kwa muda wa maisha yake yote akistaafu analipwa kiinua mgongo milioni 3. Mbunge aliyetumikia kipindi kimoja cha miaka 5 analipwa kiinua mgongo milioni 40. Je tutfika? Wataalamu wanaonekana si lolote mbele ya wanasiasa. Nini watu wanajifunza kutokana na mfumo huu?

    ReplyDelete
  9. Walimu gomeni kwani Jk. na serikali yake hawajali MASLAHI ya Nchi. Na walimu ndiyo nguzo na msingi wa elimu hatuna viongozi wenye TIJA badala yake ni MATAPELI NA WANYANYASAJI WA NCHI huku wakipeleka Raslimali zetu Nchi za nje!.. WANA AKILI HAO KWELI? WLM. GOMENI HADI BUNGENI 2012 KIELEWEKE na MUSIKUBALI KUDANGANYWA na kurudi mashuleni kiholela holela kama WATUMWA WA NCHI HII. wamewatumikisha vya kutosha so enough is enough "FOWARD EVER BACKWARD NEVER"

    ReplyDelete
  10. Naungana na wazo la kutogoma kwa waalimu la mchangiaji wa 2.12,2011 11.57 am

    WALIMU ACHENE KUTISHIA AU KUGOMA. MATOKEO YAKE NI BALAA TUPU. KWANZA TUAMBIENI MGOMO AMBAO MMEKWISHA FANIKIWA. VIONGOZI WA CHAMA CHENU WATAKUWA WANAPOKEA MISHAHARA YAO NA KUSTAREHE NYUMBANI NA KUITWA IKULU KUJADILIANA NA KUPEWA AHADI. NYIE MTABAKIA MNALIA TU.

    TUMIENI WAZO LA KURA YENU. KWANZA WATISHENI WAGOMBEA UONGOZI KWAMBA HAMTAWAPA KURA ZENU,PIA MTAWASHAWISHI WENYE MAPENZI MEMA NA NYIE KAMA TUCTA , WAZAZI,WANAFUNZI WAKIWAMO MAPROFESA, NA JAMII KWA UJUMLA. WOTE HAWA WAMMEFUNDISHWA NA WAALIMU. MARA MTAKAPOTISHIA HIVI MTAONA MATOKEO YAKE. KAMA ALIVYOSEMA MCHANGIAJI, KURA NI SILAHA INAYOOGOPWA SANA. ACHANENI NA WASHABIKI WANAOWAAMBIENI "ENOUGH IS ENOUGH FORWARD EVER BACKWARD NEVER" HAWA NEVER WATAKUWA MITAANI WAKITUMBUA NYIE MKISAGA MENO NA KULIA BAADA YA KUGOMA.

    ReplyDelete
  11. ukweli ni kuwa viongozi wa chama cha walimu ni wasaliti wakubwa,hawana lolote, wangekuwa na akili wangeenda DRC au hata hapo kenya wakaone walimu wanavyodai haki zao!! Hivi mukoba... Bado unaendelea kuwadanganya walimu kuhusu migomo!! hivi na nanyie walimu hakuna mtu mwingine anayeweza kuwaongoza? Huyu mwoga na mwongo hivyo ndiyo mnaamini atawaongoza!! kila mwaka anajidai kuitisha mgomo eti anaitisha serikali, we wadhani serikali ina watu mbumbumbu kama wewe? Wakati wenzenu wanadai nyongeza eti nyie bado mnakopwa hata mlichofanyia kazi AIBU!!, mkiendelea kuongozwa na watu kama kina Mukoba, Haiji hata siku moja mfanikiwe kwa lolote.

    ReplyDelete
  12. Mgomo ndo njia sahihi ya kutatua matatizo, kwa sababu when common senses fail, senses which are not common inatumika

    ReplyDelete
  13. mimi ni mwalimu nimekuwa nikikerwa san na cwt. niliwaza kujitoa kwa kanuni kuwa ni hiari, lkn baadae nikaona ni afadhali nikalime. lakini matokeo ni kwamba walimu wazuri wamekimbia ualimu, wanaingia walioshindwa mitihani, f4 failure, form six walioenda chuo div III na elimu ndio hio inaporomoka, chama kitabeba lawama

    ReplyDelete
  14. mchangiaji aliechangia hapo juu kwa HERUFI KUBWA, tarehe 3 jana saan 4 na dkk 28, ulichosema ni sawa, lakini usiseme kuacha mgomo, mgomo unamaana pana hata kuko kutomchagua mtu, kutompigia kura ni KUGOMA, sema kubadilisha stail ya mgomo, ona mbona mgomo wa wakati flani ulishusha kiwango cha elimu? ni kama mgomo baridi umeendelea sana hadi kesho..kikubwa ni kubadili stail ya kugoma. kumbukeni TANZANIA tumetelekezwa katika elimu tangu enzi na enzi ni tatizo la miaka na miaka. ni kuwahakikishie hata serkali wakitoa mkwara juu ya wagomaji bado mambumbumbu ndo wataogopa na kurejea kufundisha, jamani kufundisha sio njia pekee ya kutafuta maisha , usiwatishie watu kwamba kufukuzwa kazi ndio wataswaga meno sio sahihi kama umeamua kuwasaidia walimu...ujinga unawafanya walimu waendelee kunyanyashwa na hakika watabakia walimu wasiojua kufundisha kama mambo yataendelea kuwa hivi, ona RWANDA wanapewa allowance kila mwezi, walikuwa wanapewa kila baada ya miezi mitatu kama sikosei sasa wwatawekewa kila mwezi.u wa tanzania wazuri wapo kenya, rwanda, burundi, botswana, unadhani hapo nani mpuuzi.?

    ReplyDelete
  15. walimu kama serikali ingejua kuwa hata hao wanaofanya kazi za ufisadi wamefundishwa na walimu wasingefanyiwa hivyo ,jamani Taifa ilinaenda wapi na miaka 50 ya uhuru bla kujali walioleta uhuru maana aliyepigania uhuru ni hayati Mwalimu Nyerere sasa hayo yanayofanywa na serikali nini walipeni jamani walimu stahili zao.ili kuepusha madhala kwa taifa maana watoto wakishindwa kujifunza serikali inatengeneza boma ambalo likilipuka ndo serikali itaanza kusema nigelijua huja baadaye,

    ReplyDelete
  16. KUGOMA NI HAKI YAO KWA KUDAI MASLAHI YAO, LAKINI JE, WAKIGOMA ITASAIDIA? KAMA WANAONA NDIO NJIA YA KUFIKISHA UJUMBE NA KUWEZA KUSIKIKA KILIO CHAO SAWA WAGOME LAKINI KAMA IKO NJIA AMBAYO KILIO CHAO KITASIKIKA HAKUNA HAJA YA KUGOMA WAFATE HIYO NJIA MBADALA, MAANA KTK KUGOMA KUNAWANYIMA WATOTO WENGI WASIO NA HATIA HAKI YAO YA KIMSINGI NA UKIZINGATIA NI WATOTO WA WALALAHOI,NA PIA KITU KIKUBWA KILICHOZIDISHA KUCHELEWESHWA MALIPO YAO BAADHI YA WALIMU SI WAADILIFU WALIGUSHI RISITI NA MADAI AMBAYO SI HAKI YAO MUWE WAKWELI NA WAADILIFU MULIPWE, NA UONGOZI WENU MBONA ULIFIKIA MAHALI PA ZURI KATI YAO NA SERIKALI TATIZO LIKO WAPI?AU VIONGOZI WENU SI WAKWELI?FATENI NJIA SAHIHI MNA UWEZO WA KUONANA NA UONGOZI WOWOTE WA JUU ONANENI NA RAISI AKUPENI KAULI YAKE YA MWISHO HAPA TATIZO NI WATENDAJI NDIO KIKWAZO HUKO JUU KUKO SAWA LAKINI KWA KUWA WATENDAJI NI WABOVU MAANA YAKE HATA RAISI ANAHUSIKA NA UCHELEWESHAJI HUO INAKUWAJE ATOE MAELEKEZO HALAFU HAYAFATWI MAANA YAKE NI NINI?!!?

    ReplyDelete
  17. Naungana na anonymous wa 5 Dec 8.55 hapo juu.

    Waalimu MSIGOME. Itakula kwenu. Nyie ni wazazi itabidi mvumilie nakutumia busara kutafuta haki yenu. Jipimeni mna nguvu gani. Mna baki ya fedha za kuwalipa ikiwa mgomo utaendele muda mrefu? Waulizeni CWT ikiwa wana hizo fedha. Kama hawana wanawababaisha tu. Fedha wanazozikusanya wanajengea majumba makubwa makubwa, magari ya kifahari, allowances, kutoa michango ya kusaidia jamii nk. bila kujali kuwa mischango ni yenu ya kuwasaidia wakati wa shida. Hawakumbuki kuwa lazima kuwe na fungu lakusaidia wakati wa mgomo. Si hoja hawatakuwa hata na fedha za nauli za kuwasafirisha hadi maeneo ya kufanya mgomo na za posho. Mkishindwa ktk harakati zenu viongozi watabakiwa kama walivyokuwa. Wao watachota kutoka michango yenu na nyie mtakamua mifuko yenu. Hivyo hivo watakuwa mashabiki wanaowataka mgome. msitumie migomo kama siasa.

    TAFUTENI NJIA MBADALA KUDAI MAFAO AU KUTATUA MATATIZO YENU. Ziko njia nyingi mbabala kama aliyoitoa anonymous wa Dec.3/2011 4.28pm kuhusu demokrasia ya KURA. Itachukuwa muda mrefu/mfupi lakini ina matokeo mazuri ambapo walimu,wanafunzi wala wazazi hawataaumia. hakutakuwa na chki au mkwaruzo. TISHIA kwa kura yako anasema mchangiaji.

    Waalimu kumbukeni fani yenu sio sawa na ya madaktari au mapilot. Kama serikali nyingi zilivyo zitawaambia hakuna fedha kama vile mzazi wako atakavyokuambia hana fedha labda za kununua vitabu au sare. Hata kama atakuwa ametumia vibaya fedha za mshahara au pato lake vibaya kwa kununua pombe au anasa nyingine atakuambia hana fedha na ukweli hatakuwa nazo. Kama mtoto, utatafuta njia ingine mbadala labda kwenda kwa mama. Huwezi kumkataa baba au kumkata shingo. Haya yanatokea. Busara itumike na sio mgomo.

    ReplyDelete
  18. walimu kugoma mchezo mmelogwa na cwt na wanadanganya wenyewe wanapewa HELA ikulu niambieni lini mmefanikisha mgomo kila siku tunagoma mkipewa vihela kidogo mnalizika

    ReplyDelete
  19. Mgomo ni sehemu ya kudai haki! walimu Kenya walifanya hivyo na kufanikiwa sasa ni zamu ya madaktari .Utaachaje kugoma ikiwa kina Ngeleja,Jairo na wenzake wanachezea kodi zetu hali kadhalika wabunge wanalipana posho za kuketi ,kusinzia,kuzomea na kuunga mkono hoja asilimia mia moja? Ikumbukwe walimu ni walipa kodi wazuri mbali na mishahara midogo,njia ya KURA ni sawa ila inachukua muda mrefu na isitoshe chaguzi za Afrika siyo za kidemokrasia pengine tatiz moja kubwa ni kwamba CWT kwa sasa hawaaminiki ni wasanii waliweza akina Peter Lebabu Mashanga tu.

    ReplyDelete
  20. Walimu ni miongoni mwa watendaji wa serikali wenye dhima kubwa katika kuzalisha na kutengeneza kizaji cha leo na kesho chenye uzalendo na kujua utaifa wao. Leo ikiwa tunaazimish amiaka 50 ya UHURU wa Tanganyika wakati huo Walimu wanadai malipo yao na Wakati huo Wabunge wanajiongezea posho, hivi kweli tutafika? Kauli mbiu ya Tumethubutu, Tumeweza na TTunazidi kusonga mbele ingefaa sana kama madai ya Walimu nayo yangekuw yamelipwa ndio mgesema Tumethubutu, kama watu hawa hawajalipwa TUmethubutu katika lipi? Na Said Mulisa

    ReplyDelete
  21. Waalimu mna silaha nzuri sana hamjaitambua hamasisheni wanafunzi na wazazi kukimwaga chama cha CCM baaaaaaaasi mwaka 2015. Piga chini... Mtakuwa mpepata uvumbuzi baasi. Ushawishi wenu ni mkubwa sana hata kuzidi waandishi wa habari.

    ReplyDelete