Na Mwandishi Wetu, Tanga
MICHUANO ya Vyuo Vikuu nchini, imeanza kutimua vumbi katika viwanja tofauti jijini Tanga ambapo zaidi ya timu 25 za vyuo vikuu zimewasili kwa ajili ya kinyang'anyiro hicho. Akizumgumza
katika ufunguzi wa michuano hiyo, Mratibu na Mweka Hazina wa Chama cha Michezo ya Vyuo Vikuu nchini, Yussuph Omary alisema hadi sasa timu zote zimewasili ili kuleta ushindani katika michuano hiyo inayojulikana kwa jina la ''TUSA LAPF GAMES''.
Alisema michuano hiyo inafadhiliwa na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF),
kwa gharama ya sh. mil 28 italeta hamasa kubwa hasa
ikizingatiwa udhamini huo uliofanywa na mfuko huo umesaidia kupunguza
mapungufu ya Chama cha Michezo ya Vyuo Vikuu nchini (TUSA).
''Michuano ya safari hii tuna matumaini makubwa imeleta hamasa
angalia wachezaji walivyopendeza na pia wote wamekuwa na msukumo wa
kufanya vizuri kutokana na ufadhili huu ambao tunaomba udumu''alisema.
Aliitaja michezo ambayo itakuwepo katika kinyang'anyiro hicho kuwa ni
mpira wa miguu, pete, wavu, kikapu, mpira wa meza na riadha.
Kwa upande wa mgeni rasmi katika uzinduzi wa michuano hiyo ambaye ni
Meneja wa Kanda LAPF, Luyaluya Sai alisema wamefadhili michuano
hiyo ili kuhakikisha wachezaji wa vyuo kikuu wanaimarika kiafya
na kiakili ili kukuza vipaji vya michezo nchini.
''Sisi lazima tuthamini michezo kwa sababu katika nchi nyingi mfano
Brazil sehemu kubwa ya mapato yake yanatokana na michezo sasa kutokana
na hilo na sisi tumeona tuchangie juhudi za TUSA ili kuhakikisha
michezo hiyo inafanikiwa''alisema Sai.
Katika uzinduzi wa michezo hiyo kwa upande wa soka, chuo cha Ardhi kiliifunga chuo Kishiriki cha Elimu Zanzibar kwa mabao 5-1 huku chuo cha Mkwawa kikiwachabanga wenzao wa chuo Muhimbili mabao 2-1.
Katika michezo hiyo, LAPF imedhamini vifaa mbalimbali vya michezo ikiwa ni pamoja na jezi, mipira, nyavu, vikombe, medali ambapo vyote vina thamani ya zaidi ya sh. mil 28.
No comments:
Post a Comment