Na Martha Fataely, Moshi
BAADHI ya viongozi wanakwamisha maendeleo kutokana na kuegemea katika siasa, biashara na kusababisha mgongamo wa masilahi hivyo kuwafanya washindwe kutoa
maamuzi.
Bw. Madaraka Nyerere, aliyasema hayo jana mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro wakati akiongoza timu ya watu 90 kutoka ndani na nje ya nchi kupanda mlima Kilimanjaro ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru.
Alisema viongozi wengi wanakiuka maadili ya uongozi hivyo kusababisha matatizo katika utendaji kazi wa kila siku jambo ambalo linakwamisha juhudi za wananchi kujiletea maendeleo.
“Leo nimekuja kwa ajili ya kupanda mlima, sasa naona mnataka
nigeuze ajenda, yapo mambo yanatakiwa kubadilishwa, hii tabia ya viongozi kuchanganya biashara na uongozi inaleta mgongano wa masilahi, matatizo tuliyonayo leo yanachangiwa na hilo,” alisema.
Mapema akizindua safari hiyo ambayo imeandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Kampuni ya Kusafirisha Watalii ya Zara Tours , Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bw. Musa Samizi, alisema msafara huo pia unajumuisha waandishi sita wa habari.
Aliipongeza TTB, TANAPA na Kampuni ya Zara kwa kuandaa safari hiyo ili kuadhimisha miaka 50 ya uhuru pamoja na mambo mengine, safari hiyo inahamasisha utalii wa ndani ambao unaonekana kukua.
Bw. Samizi aliwataka washiriki wote kuhakikisha wanajitahidi
kufika kileleni katika siku zilizopangwa na kushuka Desemba 10 mwaka huu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Zara Tours, Bi.
Zainab Ansell, alisema kila mwaka kampuni yake itaandaa safari hiyo kwa lengo la kuutangaza ulima huo.
Alisema sekta ya utalii nchini imepata mafanikio mbalimbali ndani ya miaka 50 ya Uhuru huku amani na utulivu, ikiendelea kuwavutia wageni kutoka mataifa yote duniani.
Awali Mhariri Mtendaji wa gazeti hili, Bw. Ima Mbuguni, ambaye ni miongoni mwa waandishi sita wanaopanda mlima huo, alisema anajivunia kuzaliwa ndani ya miaka 50 ya Uhuru waakati Tanzania ikiendelea kuwa nchi ya amani na utulivu.
Aliwataka Watanzania wa kada zote pamoja na vyombo vya
habari, kutangaza mafanikio yaliyopatikana ndani ya miaka hiyo na kueleza changamoto zilizopatikana kwa kipindi hicho ili zifanyiwe kazi na kuleta maendeleo endelevu.
Akizungumzia safari hiyo, Ofisa Uhusiano wa TTB, Bw. Godfrey
Tengeneza, alisema bodi hiyo ilikusudia kuandaa ziara hiyo ili kutangaza utalii wa ndani ndani ya miaka 50 ya uhuru.
No comments:
Post a Comment