05 December 2011

Wananchi: Tafiti za APRM zifanyiwe kazi

Na Mwandishi Wetu

WANANCHI wa kada mbalimbali, watoa wito kwa Serikali kuboresha na kuinua utawala bora nchini katika miaka 50 ijayo kwa kufanyia kazi tafiti zinazofanywa na taasisi zake hasa Mpango wa
Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).

Wito huo ulitolewa kwa nyakati tofauti na wananchi waliotembelea banda la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Maonesho Maalumu ya Miaka 50 ya Uhuru yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Sabasaba, Dar es Salaam.


APRM imepewa dhamana ya kukusanya maoni ya wananchi juu ya hali ya utawala bora ili kuisaidia Serikali kufanyia kazi changamoto zinazojitokeza.

“Pamoja na kwamba bado wananchi wengi hawajaelimika kuhusu utawala bora, binafsi nimesikia kuhusu utafiti wenu hasa kuhusu namna nchi yetu inavyojenga uelewa wa wananchi ili waseme utawala bora wanaoutaka,” alisema mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu, Dar es Salaam ambaye alitembelea banda hilo.

Wananchi wengine waliotembelea banda hilo walisema ingawa Tanzania ni nchi ya amani, bado ina changamoto ya kuilinda amani hiyo kwa kutekeleza misingi ya utawala bora.

Akifafanua baadhi ya kero za wananchi, Ofisa Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania, Bw. Hassan Abbas, alisema mchakato huo ulipoanza nchini, wananchi walielimishwa kupitia mikutano iliyofanyika mijini, vijijini,  semina za makundi na vyombo vya habari.

“Kuhusu Serikali kufanyia kazi maoni ya wananchi, bado hatujafikia hatua hiyo maana katika mchakato huu, baada ya Rais kuwasilisha ripoti mbele ya wakuu wenzake wa Umoja wa Afrika, ndio anapewa michango alafu nchi inaanza kufanyia kazi maoni ya wananchi kwa miaka mitatu kabla ya kufanyika tena utafiti mwingine,” alisema.

Aliongeza kuwa, kabla ya hatua hiyo kufikiwa nchi haizuiwi kuanza kufanyia kazi maoni ya wananchi wake ambayo yametolewa katika ripoti ambayo taasisi hiyo imeikamilisha Septemba mwaka huu.

“Hapa nchini ukiangalia maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu masuala kama katiba na matakwa ya kudhibitiwa matumizi holela ya fedha katika chaguzi, haya yamefanyiwa kazi au yanaendelea kufanyiwa kazi,” alisema Bw. Abbas.

Aliongeza kuwa miaka 50 ya uhuru pamoja na changamoto zilizojitokeza, utafiti wa APRM ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika umeonesha kuwa, Tanzania ni nchi ya amani na kidemokrasia.

No comments:

Post a Comment