22 December 2011

Mkakati wa TBS utainua kipato cha Taifa

Na Daud Magesa,
Mwanza

SERIKALI Mkoani Mwanza imesema mpango wa Shirika la Viwango  (TBS) kuanzisha mkakati wa udhibiti wa bidhaa zisizokidhi viwango vya ubora,zinazoingizwa nchini utasaidia kuinua pato la taifa, kulinda ajira na afya za walaji hasa masikini Watanzania.


Mkakati huo pia utaongeza ushindani sawa wa kibiashara kati ya bidhaa zenye ubora zinazozalishwa na nchini na zinazotengezwa na viwanda na kampuni
za nje.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo,wakati akifungua mkutano wa wadau wa TBS, ambao ulifanyika hivi karibuni.

Alisema kuwa mpango huo utawezesha kulindwa kwa ajira na kuimarisha viwanda vya ndani viweze kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi viwango vya kimataifa ili kulinda afya za walaji ambao ni masikini wa Watanzania na kuongeza uwekezaji wa ndani.

“Kuruhusu bidhaa isiyo na ubora ni tishio,kwa sababu afya za walaji zitaathirika.Lakini pia bidhaa hizo zinaharibu mazingira yetu kwa nchi kugeuka kuwa jalala la bidhaa hizo zisizo na ubora, ambapo nchi wazalishaji wataendelea
kututupia bidhaa zao, hivyo ni bora tuzidhibiti huko kwao kabla ya hazijaingizwa nchini,” alisema

Alisema kuwa bidhaa nyingi zenye ubora wa chini zimezagaa sokoni hali inayochangia kuikosesha serikali mapato kutokana na bidhaa hizo ambazo huingizwa kwa njia za panya hasa katika mipaka yetu.

Mkuu huyo wa mkoa aliwataka watendaji wa kampuni yaliyopewa zabuni ya kufanya ukaguzi huo kufanya kazi kwa uaminifu kwa vile yamepewa dhamana ya kulinda afya za
Watanzania.

Awali akimkaribisha Mkuu huyo wa Mkoa kwa niaba ya Mkurugenzi wa TBS Bw. Charles Ekelege, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa shirika hilo, Bi.Kezia Mbwambo alisema kuwa ukaguzi bidhaa utafanywa katika nchi zinakotoka, ili kuhakikisha bidhaa
zinazoingizwa nchini ni zenye ubora unaokidhi viwango vya ubora kimataifa.

No comments:

Post a Comment