15 December 2011

Ufaulu waongezeka

*Asilimia 90.1 wachaguliwa kwenda secondari.
*Zaidi ya wanafunzi 9,000 wafutiwa matokeo.
*Waliofaulu kupimwa kujua kusoma, kuandika.
*Walimu wakuu, wasimamizi wakalia 'kuti kavu'.

Na Rehema Maigala

BARAZA la Mitihani la Taifa (NECTA), limefuta matokeo ya watahiniwa 9,736 waliofanya mtihani wa kumaliza
darasa la saba mwaka huu baada ya kubainika kufanya udanganyifu. Pia wanafunzi 567,567 kati ya 983,545 waliofanya mtihani huo ambapo wanafunzi 515,187 sawa na asilimia 90.1 wamechaguliwakuingia kidato cha kwanza katika shule za sekondari za Serikali. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bw.Philipo Mulugo, alisema
licha ya wanafunzi 567,567 kufaulu mtihani huo, Serikali inaendelea na uchunguzi ili walimu waliohusika na udanganyifu wachukuliwe hatua za kisheria. Alisema kati ya wanafunzi waliobainika kufanya udanganyifu wapo wavulana 4,943 na wasichana 4,793. Alitaja aina za udangayifu waliofanya kuwa ni pamoja na watahiniwa 94 kukutwa na karatasi na rula zenye majibu pamoja na viatu aina ya ‘yeboyebo’, zikiwa na majibu ya mtihani. Alisema wanafunzi hao walikamatwa katika Halmashauri za Bukoba mkoani Kagera, Muheza mkoani Tanga, Maswa mkoani Shinyanga, Sumbawanga mkoani Rukwa, Mtwara, Lindi na Tarime mkoani Mara. Alisema udanganyifu mwingine umefanywa na watahiniwa wanne ambao waliandikiwa majibu katika karatasi za mtihani. “Aina ya tatu ya udanganyifu ni watahiniwa tisa kurudia darasa la saba kinyume na taratibu pamoja na watahiniwa 9,629 waliokuwa katika chumba kimoja cha mtihani kuwa na mfanano wa makosa yasiyo ya kawaida,” alisema. Aliongeza kuwa, kutokana na udanganyifu huo, Serikali imedhamiria kufanya uchunguzi na kuhakikisha wote waliohusika wanachukuliwa hatua stahiki. Bw.Mulugo alisema, hatua za kinidhamu pia zitachukuliwa kwa shule zote zilizohusika katika udanganyifu huo. Alisema kati ya wanafunzi waliofaulu, wasichana 253,402 sawa na asilimia 49.1 na wavulana 261,785 sawa na asilimia 50.9 ambapo
idadi hiyo imeongezeka kwa asilimia 12.49 kutoka wanafunzi 456,350 mwaka 2010. Aliongeza kuwa, pamoja na ongezeko hilo la ufaulu, wanafunzi wengi watakosa nafasi kutokana na ufinyu wa shule ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, wanafunzi 7,000 watakosa nafasi za kwenda shule za serikali. Akizungumzia malalamiko ya kuwepo kwa wanafunzi wanaofaulu mtihani huo bila kujua kusoma na kuandika, Bw.Mulugo alisema wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza, watafanya mtihani wa kujipima kabla ya kuanza masomo. “Mwanafunzi ambaye itabainika amejiunga na kidato cha kwanza bila kumudu stadi husika, Mwalimu Mkuu wa shule aliyotokea mwanafunzi na msimamizi wa mtihani watachukuliwa hatua za kinidhamu," alisema.

1 comment:

  1. hii ni kujiongezea gharama na kutumia kodi za walalahoi kinyume, kusoma na kuandika wakati unafanya huo mtihani wa darasa la saba tayari inakuwa inapimwa , ikiwa mwanafunzi kapasi kiwango kinachotakiwa , ina maana aliweza kusoma swali na kujibu kwa kuandika, tusijiongezee gharama na pia kuwaumiza wanafunzi wetu kisaikolojia kwa mitihani isiyo na tija. Mwanafunzi wa darasa la pili tayari anakuwa anajua kusoma na kuandika , vipi unataka kumtahini tena kwa hilo? au kuna ulaji unapangwa? Kama kawaida yetu tunataka posho , sitting allowance nk. Acheni mambo yenu ya kipuuzi.

    ReplyDelete