06 December 2011

TBF yaitaka mikoa kusapoti timu zao

Na Mwali Ibrahim

SHIRIKISHO la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), limeitaka mikoa itakayoshiriki mashindano ya Taifa,
kutoa sapoti kwa timu zao zishiriki vyema michuano hiyo.

Mashindano hayo yanatarajia kufanyika Desemba 11, mwaka huu katika viwanja vya Leaders Kinondoni na Don Bosco Upanga, Dar es Salaam ambayo yataenda sambamba na kusheherekea miaka 50 ya Uhuru Tanzania Bara.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Msaidizi wa TBF Michael Maluwe, alisema kama mikoa itatoa sapoti ya kutosha kwa timu zao itawasaidia kuwa na uhakika wa timu zitakazoshiriki mashindano hayo na hasa katika upangaji wa ratiba.

"Tunaitaka mikoa izisapoti timu zao, ili kuturahisishia kupanga ratiba kwani timu zinaweza kuthibitisha lakini kwa kukosa sapoti ya mikoa yao, inaweza kushindwa kufika katika mashindano na kuleta usumbufu kwenye upangaji wa ratiba kutokana na kukosa fedha za kuwawezesha kufika katika mashindano," alisema Maluwe.

Alisema maandalizi yanaendelea, ambapo hadi sasa hakuna mikoa iliyoongezeka kuthibitisha kushiriki mashindano hayo na kufanya idadi kubaki mikoa 17 iliyothibitisha hadi sasa.

Aliitaja mikoa iliyothibitisha kuwa ni Morogoro, Arusha, Mwanza, Mbeya, Rukwa, Mara na Mtwara ambazo tayari zimeshatuma majina ya timu zao huku kila timu ikiwa na wachezaji 12 na mikoa ya Kilimanjaro, Tabora, Shinyanga, Unguja na Pemba zimetoa timu mbili kwa kila mkoa na kusajili wachezaji 24, watakaoshiriki mashindano hayo.

Mkoa wa Dar es Salaam umetoa timu sita kutoka Wilaya za Temeke, Ilala na Kinondoni ambapo kila wilaya imetoa timu mbili na wachezaji 24 kwa kila timu.

No comments:

Post a Comment