Rehema Mohamed na Zena Mohamed
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewataka mawakili wa utetezi na wa Jamhuri katika kesi ya wizi wa sh. bilioni 2.2 katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu ya Tanzania
(EPA) inayomkabili Bw. Rajabu Maranda, na mwenzake kutochelewesha usikilizwaji wa shauri hilo.
Hayo yalisemwa mahakamani hapo jana na mmoja wa jopo la mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo Hakimu Katarina Revocati wakati kesi hiyo ilipofikishwa mbele ya mahakama hiyo kwa ajili ya kuanza kusikilizwa huku upande wa utetezi unaoongozwa na wakili, Bw. Majura Magafu, akikosekana mahakamani na kutoa taarifa ya kutokuwepo kwa kutuma barua.
Alisema Bw. Magafu anatakiwa kutoa taarifa za udhuru mapema na kwamba kuchelewa kufanya hivyo kunachelewesha usikilizwaji wa kesi hiyo huku akijua kuwa mwenyekiti wa jopo la mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo Jaji Fatuma Masengi amehamishiwa Arusha kikazi.
"Hatujui Magafu alipata lini taarifa za kwenda Tanga, awe anasema mapema, anajua fika kuwa Jaji amehamishiwa Arusha hivyo anatumia gharama kuja na kuondoka, kuna siku upande wa utetezi utalazimika kulipia gharama," alionya Bi. Revocati
Awali Wakili wa Serikali Mkuu, Bw. Fedrick Manyanda, alitoa taarifa ya kutokuwepo kwa wakili huyo kwa madai kuwa amekwenda Tanga kuhudhuria kesi.
Alidai kutokana na hali hiyo wanaomba tarehe nyingine ya kutajwa ili kupanga tarehe ya kuanza kusikilizwa utetezi hivyo mahakama hiyo kulazimika kupanga Januari 30, mwakani.
Katika kesi hiyo, Bw. Maranda na mshtakiwa mwenzake Bw. Farijara Hussein wanadaiwa kuiibia BoT zaidi ya sh. bilioni 2.2 baada ya kudanganya kuwa Kampuni yao ya Money Planners & Consultant imepewa idhini ya kudai deni BoT na Kampuni ya B. Grancel ya nchini Ujerumani huku wakijua si kweli.
No comments:
Post a Comment