Na Mwali Ibrahim
KLABU za mpira wa wavu za KAVC, KCC za Uganda na NCC, KPLC, KBC, STIMA na Youth za Kenya zimethibitisha kushiriki michuano ya kimataifa ya Kombe la Nyerere
(Nyerere Cup), inayotarajia kufanyika Desemba 15 hadi 18, mwaka huu katika viwanja vya Hindumandal Moshi.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya mchezo huo Tanzania, Alfred Selengia alisema maandalizi ya mashindano hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Wavu Tanzania (TAVA), yanaendelea ambapo timu nyingi zimejitokeza kushiriki.
Alizitaja klabu za Tanzania zilizothibitisha kuwa ni Jeshi Stars, Magereza, JKT, Shule za Sekondari za Makongo na Loard Baden Powel, Kijichi, Tanga Central, Rukwa, Moshi University, KCMC University nyingine ni Mafunzo, Nyuki na Polisi za Zanzibar.
"Upinzani utakuwa mkubwa mno kwa kuwa klabu zilizothibitisha ni nyingi na nafasi bado zipo kwa nyingine zitakazohitaji kushiriki mashindano haya," alisema Selengia.
Selengia amezitaka timu kutumia muda uliopo kwa ajili ya kujiandaa na kuonesha upinzani wa kutosha katika kutafuta ushindi kwenye mashindano hayo.
Amezitaka pia timu za Tanzania kuhakikisha zinajiandaa vya kutosha, kuchukua ubingwa huo kutokana na mashindano hayo kufanyika nchini hivyo kuhakikisha ubingwa unabaki hapa nchini.
No comments:
Post a Comment