Z'bar Heroes, Rwanda mtifuano leo
*Burundi kuikabili Sudan *Viingilio vyaongezeka
Na Zahoro Mlanzi
ROBO fainali ya michuano ya 35 ya Kombe la Tusker Chalenji, inatarajiwa kuanza leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kupigwa
mechi mbili kati ya Burundi itakayoumana na Sudan ikifuatiwa na Zanzibar Heroes itakayotoana jasho na Rwanda 'Amavubi'.
Mbali na hilo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeongeza viingilio vya michuano hiyo ambapo cha chini kitakuwa ni sh. 2,000 badala ya sh. 1,000 na cha juu ni sh. 15,000 badala ya sh. 10,000.
Macho na masikio katika mechi za leo yataelekezwa katika mchezo kati ya Zanzibar na Rwanda ambao ndio unaovuta hisia za watu wengi kutokana na timu hizo kucheza mchezo unaofafana huku baadhi ya wachezaji wa timu hizo wakijuana vizuri.
Rwanda ambayo mwaka uliopita iliondolewa katika hatua ya robo fainali na Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) kwa kufungwa bao 1-0, imefuzu hatua hiyo baada ya kushinda mechi zake zote za Kundi A na kuwa kinara wa kundi hilo kwa kufikisha pointi tisa.
Timu hiyo ilianza michuano hiyo kwa kumchapa bingwa mtetezi, Kili Stars kwa bao 1-0, ikaifunga Zimbabwe mabao 2-0 na kumalizia na Djibouti kwa kuichapa 5-2, hivyo kujikuta ikikata tiketi ya robo mapema.
Kwa upande wa Zanzibar Heroes, yenyewe imefuzu robo fainali ikishika nafasi ya tatu kutoka Kundi B kwa kuwa na pointi nne lakini iliingia hatua kama 'best looser' baada ya kuwa na pointi na uwiano wa magoli ambayo timu nyingine zilizofanya vibaya hazikufikisha.
Zanzibar Heroes ilianza kwa kucheza na Uganda 'The Cranes' ambapo ilifungwa mabao 2-1, ikacheza na Somalia ilipata ushindi wa mabao 3-0 na kumalizia kwa kutoka sare na Burundi, hivyo ikafikisha pointi nne.
Mbali na hilo, burudani ya aina yake itakuwepo kwa kiungo wa Rwanda, Haruna Niyonzima ambaye atakuwa na kazi ya ziada atakapochuana na Abdulhalim Humud wa Zanzibar pamoja na beki, Nadir Haroub 'Cannavaro' ambao watakuwa na kazi ya ziada kuhakikisha haleti madhara.
Robo fainali nyingine ambayo itaanza saa nane mchana itazikutanisha Burundi na Sudan ambapo Burundi imetinga hatua hiyo baada ya kuongoza Kundi B kwa kufikisha pointi saba na Sudan ikishika nafasi ya pili kutoka Kundi C.
Katika hatua nyingine, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeongeza viingilio vya mechi zote za robo fainali ambapo sh. 2,000 kwa viti vya kijani na bluu, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B na sh. 15,000 kwa VIP A.
Taarifa hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura kwa vyombo vya habari.
Robo fainali zingine zitachezwa kesho kwa kuzikutanisha Uganda itakayoumana na Zimbabwe ikifuatiwa na Tanzania Bara itakayoumana na Malawi katika mechi zitakazopigwa kwenye uwanja huohuo.
No comments:
Post a Comment