05 December 2011

Mkwassa:Tutafanya vizuri hata tukizomewa

Na Zahoro Mlanzi

BAADA ya kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Tusker Chalenji, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Charles Boniface Mkwassa, amesema
watafanya vizuri katika hatua inayofuata licha ya kwamba kuna watu wanaizomea timu yake.

Hali hiyo ya kuizomea Kili Stars imekuwa ikijitokeza hasa timu hiyo inapokuwa haifanyi vizuri katika mechi zake na hata katika mchezo wa juzi uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Zimbabwe baadhi ya mashabiki walisikika wakizomea.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo ambao Kili Stars ililala kwa bao 2-1, Mkwassa alisema hawezi kumlazimisha mtu kuishangilia Kili Stars lakini anaamini ipo siku wenyewe bila kushurutishwa wataishangilia.

“Hilo ni jambo la kawaida kutokea katika soka, huwezi kumlazimisha punda kunywa maji lakini naamini kuanzia robo fainali, timu itazidi kuimarika na kupata matokeo mazuri,” alisema Mkwassa.

Akizungumzia mchezo dhidi ya Zimbabwe, alisema vijana walijituma kadri ya uwezo wao lakini ndio hivyo matokeo yamewahukumu kwani bahati haikuwa yao.

Alisema walitarajia kupata ushindani katika mechi hiyo na kweli mechi ilikuwa ngumu kwa upande wao lakini wanashuku wamevuka kwa utofauti wa mabao.

Mbali na hilo, alizungumzia pia mabao waliyofungwa, alisema wamefungwa kutokana na makosa madogo madogo lakini makosa hayo atayafanyia kazi ili kuwapa raha watanzania.

Akizungumzia mchezo wa robo dhidi ya Malawi ambao utapigwa kesho, Mkwassa alisema ni timu ngumu hivyo wataendelea kurekebisha makosa ambayo yamejitokeza katika mechi zilizopi ili kuhakikisha wanasonga mbele.

No comments:

Post a Comment