Na Zahoro Mlanzi
TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (Ngorongoro Heroes), leo itashusha
karata ya mwisho ya kuwania ubingwa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu kwa nchi za Kusini mwa Afrika (COSAFA), kwa kuumana na Mauritius katika mchezo utakaopigwa Uwanja wa Molepolole, Botswana.
Ngorongoro Heroes ambayo ipo Kundi C, pamoja na timu za Afrika Kusini na Zambia, mpaka sasa haijashinda mechi zake mbili za awali.
Ilianza kwa kuumana na Zambia, ambapo ilitoka sare ya mabao 3-3 na juzi kulazimishwa sare nyingine ya bao 1-1 dhidi ya Afrika Kusini, hivyo kuifanya ifikishe pointi mbili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na COSAFA jana, timu hiyo inashiriki michuano hiyo kama timu mwalika, inabidi washinde mchezo huo wa leo ili ijiweke katika nafasi nzuri ya kusonga mbele, huku mechi nyingine ya mwisho ya kundi hilo itazikutanisha timu za Afrika Kusini, itakayoumana na Zambia.
Katika mchezo wa leo, Ngorongoro Heroes itamkosa mchezaji wake mahiri, Issa Rashid baada ya mchezo dhidi ya Zambia kuoneshwa kadi nyekundu kutokana na kuunawa mpira makusudi.
Zambia ndiyo bingwa mtetezi wa mashindano hayo, baada ya kuifunga Namibia 4-1 katika mechi ya fainali iliyopigwa mwaka jana.
No comments:
Post a Comment