Na Zahoro Mlanzi
WAKATI michuano ya Kombe la Tusker Chalenji ikiendelea, Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA),
imeipiga faini ya dola 200 timu ya taifa ya Malawi kwa kuchelewa kufika katika vikao vya mechi.
Timu zote ambazo zimetinga robo fainali ya michuano hiyo, ambayo ilianza jana zilikuwa na kikao hicho juzi mchana katika hoteli moja katikati ya jiji, lakini timu hiyo haikutokea bila ya kuwa na sababu za msingi.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa baraza hilo Nicholaus Musonye, alisema timu hiyo ambayo ni mwalikwa imekumbana na adhabu hiyo, baada ya kuchelewa kufika kikaoni na hata ilipoongezewa muda ilishindwa kutokea.
“Timu hiyo italazimika kulipa dola 200 kabla ya kukutana na Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), katika mchezo utakaopigwa kesho (leo), kama ikishindwa kufanya hivyo kwa wakati watajua la kufanya,” alisema Musonye.
Katika hatua nyingine, Musonye alisema katika hatua hiyo ya robo fainali dakika 90, zikimalizika ni penalti moja kwa moja na wala hakutakuwa na dakika za kuongeza.
Aliongeza kwa kutoa onyo kwamba timu yoyote, itakayokuwa ikipoteza muda bila ya kuwa na sababu za msingi itachukuliwa hatua kwa kuwa hakuna shabiki atakayekubali mpira ukose, ladha kwa timu fulani kufanya kisichotarajiwa.
Alisema kwa mchezaji ambaye amepewa kadi ya njano katika hatua ya makundi, ataruhusiwa kucheza lakini kwa wale walioonesha kadi mbili za njano na nyekundu moja kwa moja, hawataruhusiwa kucheza.
Musonye alisema dakika za ziada zitaongezwa katika hatua ya robo fainali endapo kama kutakuwa na sababu zisizoeleweka kama kunyesha kwa mvua, ambayo italazimu mchezo kusimamiashwa wakati mpira unaanza.
No comments:
Post a Comment