27 December 2011

Mganga Mkuu Misungwi atimuliwa kazi

*Adaiwa kuhusika na ubadhirifu mil. 335.5/-

Na Daud Magesa, Mwanza

HALMASHAURI ya Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, imemfukuza kazi Mganga Mkuu wilayani humo, Dkt.Daniel Nyambega, kwa ubadhirifu wa
fedha sh.milioni 335.5 kati ya sh.milioni 469.4 zilizotengwa kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya hiyo na kutekeleza miradi 21 ya vituo vya afya na zahanati chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM).

Kutokana na ubadhirifu huo, Dkt.Nyambega anadaiwa kukwamisha miradi 10 kati ya 21 ishindwe kutekelezwa licha ya kuwekwa katika mipango.

Uchunguzi uliofanywa na Majira umebaini kuwa, ubadhirifu huo ulifanyika katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita mwaka wa fedha wa 2008/2009 na 2010/2011 ambapo zaidi ya sh.milioni 469.3
zilitolewa na Serikali kwa ajili ya kutekeleza mpango huo.

Fedha zilizotumika katika mpango huo zilikuwa sh.133.8 ambapo sh.milioni 335.5 ziliishia mifukoni mwa baadhi ya viongozi na maofisa wa halmashauri hiyo.

Tume maalumu ya uchunguzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), ilibaini kuwa miradi iliyotekelezwa ilitumia sh.milioni 133.8 ambayo ni ya Hospitali ya Wilaya Misungwi, Zahanati za Mwaniko, Mwamazengo, Kanyerere, Mwawile, Gambajiga na Mwanangwa wakati Vituo vya Afya vya Koromije na Mbarika utekelezwaji wake unatia mashaka.

Chanzo chetu cha habari kilisema kuwa, tume hiyo ilibaini kuwa fedha hizo zimeliwa na wajanja hivyo kusababisha halmashauri hiyo ishindwe kutekeleza miradi ya MMAM.

Kilisema utekelezwaji wa baadhi ya miradi hiyo nao unatia mashaka na hakuna sababu zilizotolewa kwa nini miradi mingine imeshindwa kutekelezwa wakati fedha zilikuwepo.

Kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi huo, miradi ya zahanati 10 ambayo haikutekelezwa na fedha zake kutafunwa na vigogo wa halmashauri ni Mwamboku sh.milioni 47.9, Nyabumanda sh.milioni 20.8, na Nyamijundu sh.milioni 35.

Mingine ni Hospitali ya Wilaya hiyo sh.milioni 86.1, Zahanati ya Ntulya sh.milioni 11.5, Mwaniko sh.milioni 30, Isesa sh.milioni 30, Lubili sh.milioni 15.6, Nyamainza sh.milioni 13.1 na sh. milioni 42.9 zilizotengwa kwa ajili ya gharama za usimamizi.

Baada ya tume hiyo kukamilisha uchunguzi wake, ilipendekeza maofisa sita wa halmashauri hiyo wakiwemo waganga wawili (majina tunayo), wawajibike kwa kuisababishia hasara Serikali na kushindwa kusimamia agizo namba 8 (a-d).

Majira lilipomtafuta kwa njia ya simu Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Xavery Tiluselekwa, alikiri kutokea ubadhirifu huo na kuongeza kuwa, tayari Dkt.Nyambega amefukuzwa kazi.

“Kweli kuna tume ya wakaguzi ilifika na kufanya kazi yake, lakini taarifa yao sijaipata, ingawa kuna baadhi ya watumishi wamesimamishwa kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za ubadhirifu, lakini Mganga Mkuu wa Wilaya, Dkt.Nyambega ametimuliwa kazi tangu Septemba mwaka huu,” alisema Bw.Tiluselekwa.





No comments:

Post a Comment