27 December 2011

DC kumweleza JK ubabaishaji bei ya korosho

Na Steven Augustino, Tunduru

WAKUU wa mikoa inayolima zao la korosho nchini, wameazimia kufikisha kilio chao kwa Rais Jakaya Kikwete juu ya ubabaishaji wa bei ya zao hilo ili aweze kutoa tamko
kwa lengo la kuwawezesha wakulima kupata matunda ya jasho lao.

Mikoa hiyo ni Ruvuma, Lindi na Mtwara ambapo ubabaishaji huo unadaiwa kufanywa na wanunuzi wakubwa na kuwaacha wakulima wakiteseka bila msaada wa Serikali yao.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw.Saidi Mwambungu, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wadau wa maendeleo katika kikao cha dharura kilicholenga kujadili ubabaishaji huo.

“Maamuzi haya yamefikiwa na wakuu wa mikoa minne ambayo nimeitaja, Serikali haiwezi kulifumbia macho suala hili na kuwaacha wakulima wakiteseka,” alisema Bw.Mwambungu.

Kikao hicho kiliazimia kusimamisha mauzo ya zao hilo kwa kampuni zinazofanya ubabaishaji huo vinginevyo wakubali kununua kwa bei ambayo itakubaliwa.

Wajumbe wa kikao hicho, walitumia fursa hiyo kumuomba Meneja wa Benki ya NMB, Tawi la Tunduru, Bw.Omari Mleche, kuongeza mkopo kwa vyama vya msingi ili viweze kununua korosho zote kwa wakulima wakati juhudi za kutafuta soko la uhakika zikiendelea.

Awali wakitoa taarifa ya ubabaishaji wa soko la zao hilo, Meneja wa Chama Kikuu cha Wakulima wa Korosho (TAMCU Ltd), Bw.Imani Kalembo na Mwenyekiti wa chama hicho Bw.Mahamudu Katomondo, walisema ubabaishaji huo umejitokeza katika minada mitatu ambayo ilifanyika hivi karibuni.

“Kampuni ya Abbas Eport Treding Co.Ltd na Olam Co.Ltd, ziliomba kununua korosho chini ya sh.1,500 kwa kilo moja, hali hii ilionesha kampuni hizi zina ajenda ya siri ya kutaka chama chetu kishindwe kuwalipa wakulima malipo ya awamu ya pili.

“Jambo linalotupa shaka zaidi ni kitendo cha kampuni hizi kati ya 70 ndiyo zilijiandikisha na kuomba kununua korosho katika msimu wa mwaka 2011/12,” walisema.

Wakizungumzia taarifa ya ununuzi wa zao hilo kutoka kwa wakulima, walisema hadi sasa vyama vya msingi vya ushirika vimekusanya zaidi ya kilo milioni 4.5 kati ya milioni saba zinazotarajiwa kununuliwa na chama chao.

Akitoa maoni yake, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Mhandisi Ramo Makani, aliiomba Serikali itumie fedha zilizoidhinishwa katika bajeti iliyopita kwa ajili ya matumizi ya dharura ili zitumike kununua korosho za wakulima.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ligunga, Bw.Madiewani Kazembe na Bw.Burhani Nakanje wa Kata ya Marumba, walisema kiwanda cha kubangulia korosho wilayani humo ambacho kinamilikiwa na Kampuni ya Korosho Africa Ltd, hakina msaada wowote kwa wakulima.

Waliiomba Serikali kuwa macho na wanunuzi hao vinginevyo wananchi watakosa imani na Serikali yao.

Wakijibu tuhuma hizo, wasimamizi wa kiwanda hicho, Bw.Dinesh Poojali na Mhandisi wa kiwanda, Bw.Sivan Edayath , walisema mbali ya kutoa taarifa kuwa kiwanda chao kimefungwa kutokana na kuishiwa korosho, hawana maamuzi yoyote juu ya ununuzi wa zao hilo katika vyama vya ushirika vya wakulima wilayani humo.




No comments:

Post a Comment