27 December 2011

Diwani CHADEMA apigwa kisu, alazwa

*Mtuhumiwa ni mpenzi wake, kiongozi wa chama

Na Mwandishi Wetu, Mvomero

DIWANI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Kata ya Mtibwa, Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro, Bi.Tusekile Mwakyoma (28), amechomwa
kisu chini ya ziwa la kushoto na mchumba wake Mkurugenzi wa Mafunzo na Uenezi wa chama hicho, Bw.Songa Mgweno, mkazi wa Kijiji cha Kilimanjaro, ambaye alitoweka baada ya tukio hilo.

Akizungumza na Majira akiwa wodini katika Hospitali ya Misheni Bwagala, Bi.Mwakyoma alisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana ambapo Bw.Mgweno, alikimbia na fedha zake sh.200,000.

“Huyu Bw.Mgweno ambaye ni mchumba wangu, alinipigia simu saa mbili usiku niende nyumbani kwake Kijiji cha Kilimanjaro ili nikachukue fedha zangu, niliamua kulala huko na ilipofika alfajiri, aliniamsha na kuniuliza nimefanya juhudi gani kuhakikisha wazazi wangu wanakubali anioe lakini nilimwambia sina jibu.

“Tuliendelea kulala lakini baada ya muda, alianza kunipapasa nikasikia maumivu makali chini ya ziwa la kushoto, baada ya kujichunguza, nikaona kisu kikining'inia,” alisema.

Aliongeza kuwa, Bw.Mgweno alimkaba koo na kuchomoa kisu hicho ili ampige kingine lakini alijitahidi kumdhibiti huku akipiga kelele kuomba msaada ambapo ndugu wa mwanaume waliamka na kwenda chumbani kwao kutoa msaada.

“Walipofika chumbani, walikuta Bw. Mgweno tayari amekimbia kupitia mlango wa nyuma,” alisema Bi. Mwakyoma.

Kwa upande wake, mpelelezi wa makosa ya jinai mkoani hapa, Bw.Hamisi Selemani, alisema jeshi la polisi linaendelea kumtafuta mtuhumiwa ili aweze kufikishwa mahakamani.

Mama wa Bi.Mwakyoma ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja, alisema walimkataza mtoto wao asiendeleze uhusiano na Bw.Mgweno kwa sababu alikuwa na uhusiano na mwanamke mwingine ambaye ni kabila lake.

Baadhi ya wapiga kura katika kata hiyo, wamewaomba viongozi wa CHADEMA Taifa kumfukuza uanachama Bw.Mgweno kutokana na kosa alilofanya la kumshambulia diwani wao na kutaka kumuua.



No comments:

Post a Comment