*Burundi hiyoo yatangulia
Na Zahoro Mlanzi
PAMOJA na timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) jana, kuichapa Somalia mabao 3-0 haina budi kusubiri mechi za
mwisho za makundi mengine, ili kufuzu robo fainali ya michuano ya Tusker Chalenji inayoendelea Dar es Salaam.
Mechi hiyo ilipigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa nane mchana ikifuatiwa na nyingine kati ya Burundi na Uganda 'The Cranes', iliyomalizika kwa Burundi kuibuka na ushindi wa bao 1-0 na kupata tiketi moja kwa moja ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo.
Kwa ushindi huo wa Zanzibar, umefanya ishike nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi nne, huku Burundi ikipanda kileleni kwa kufikisha pointi saba na Uganda ikiwa ya pili kwa pointi sita wakati Somalia inashika mkia.
Zanzibar inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kutinga robo fainali kwa kuwa ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, ikilinganishwa na timu nyingine za makundi yaliyobaki.
Kundi A linaongozwa na Rwanda yenye pointi sita, ikiwa na mabao matatu ya kufunga ikifuatiwa na Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), yenye pointi tatu sawa na Zimbabwe ila zinatofautiana kwa mabao na Djibouti inashika mkia.
Kundi lingine linaongozwa na Malawi, yenye pointi nne ikifuatiwa na Kenya 'Harambee Stars', yenye pointi tatu, Sudan ya tatu kwa pointi mbili na Ethiopia inashika mkia ikiwa na pointi moja.
Kulingana na ratiba ya michuano hiyo, leo kwenye uwanja huohuo kutakuwa na mechi kati ya Kenya itakayoumana na Sudan na Ethiopia itacheza na Malawi na kesho Kilimanjaro Stars itaumana na Zimbabwe, ambapo matokeo ya mechi hizo ndiyo yatakata mzizi wa fitina.
Katika mchezo kati ya Zanzibar Heroes na Somalia, mabao ya Zanzibar yalifungwa na Kassim Selemani, Aggrey Morris na Amir Hamad huku bao pekee la Burundi katika mechi ya pili lilifungwa na Amissi Cedric.
Zanzibar kama wangekuwa makini wangefunga mabao mengi, lakini safu yao ya ushambuliaji iliyoongozwa na Hamad ilikuwa haijakaa sawa kwani kipindi cha kwanza, walitengeneza nafasi tatu za wazi lakini walishindwa kuzitumia.
Kipindi cha pili, pia Zanzibar Heroes walitawala mchezo kwa kiasi kikubwa, lakini kukosa umakini kumewafanya kupoteza nafasi nyingi, huku Somalia yenyewe ilionekana zaidi kutaka 'kufa' na Zanzibar kwani walicheza kwa kujiamini.
No comments:
Post a Comment