Na Bryceson Mathias, Mvomero
MKAZI wa Kitongozi cha Ifumbo wilayani hapa, Bi. Selina Jovini, amejifungua mtoto wa kike chini ya mti wa muembe baada ya kubebwa umbali wa kilomita 10 kufuata zahanati
kutokana na ukosefu wa barabara.
Mzazi wa Bi. Jovini Bw. Jovini Victor (54), alikiri mwanaye kujifungua chini ya mti huo baada yeye mwenyewe akisaidiana na wasamari wema kumbeba kwa umbali huo na kwamba tukio hilo lilitokea saa 10 usiku Desemba 23, mwaka huu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi katika kitongoji hicho Bw. Victor alisema baada ya kuvuka mabonde, milima na mito miwili mwanae alimuomba mama yake mzazi wazungumze kwanza pembeni.
Alisema baada ya kusikia ombi hilo kama mzazi alitumia hekima kwa kuwaachia nafasi na baada ya muda mfupi alisikia sauti ya mjukuu wa kike chini ya mwembe huo.
“Niliwalaani viongozi wanaowazuia wananchi wa Ifumbo wasichimbe barabara ili kufikisha kilomita 10, wamebakiza kilomita mbili kufika zahanati ya Mvomero ambako tulikuwa tukienda kwa kutembea, "alisema Bw. Victor.
Kwa upande wake mama aliyejifungua alisema kikubwa anawashukuru wazazi wake na wasamaria wema waliomsaidia kumbeba na kukosa usingizi kuelekea kwenye zahanati ambako hakufanikiwa kufika.
Pia alimshukuru Mungu kumfanikisha uzazi salama huku akiwatupia lawama viongozi wa wilaya hiyo kwa madai ya kushindwa kutatua kero ya barabara ili kuwaunganisha na zahanati ya Mvomero.
Naye Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mvomero Bw. Maiko Mzimba, licha ya kuthibitisha tukio hilo alisema ni wakati muafaka kwa serikali ya wilaya hiyo kutatua kero ya barabara hiyo.
No comments:
Post a Comment