27 December 2011

Waanza kuchangishana kujenga barabara

Na David John

WANANCHI wa Kata ya Ukonga Manispaa ya Ilala Dar es salaam, wameamua kuchangishana fedha ili kukarabati barabara yao iliyosombwa na  mvua kubwa hivyo kutenganisha
eneo la Kinyerezi na Segerea.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao jana, Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia ukarabati huo Bw. Benjamini Kilamatu, alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kutoona wanazidi kuthirika kutokana na kukosekana kwa mawasiliano kati ya maeneo hayo mawili yanayotemeana kimahitaji.

Alisema pia hawajaona hatua zozote za wazi zinazochukuliwa na Halmashauri ya Ilala tangu kutokea kwa maafa hayo jambo linalowafanya waingiwe na hofu kama watasaidiwa na serikali.

Alisema kila mwananchi ambaye anaishi katika eneo hilo amelazimika kuchangia sh. 50,000 hadi 10,000 ili kuweza kufanya ukarabati huo ambapo sehemu kubwa ya Daraja imeharibika.

Aliongeza kuwa baada ya kutokea uhalibifu huo viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli, walifika eneo hilo kujionea hali halisi.

"Wananchi tumepata shida kiasi kwamba hata huduma muhimu tunashindwa kuzifikia ikiwa pamoja na Hospitali, Gharama za maisha zimekuwa juu mara mbili kwa sababu ya barabara,"alisema Bw. Kalamatu.

kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Mongo Landege  Bw. Omari Mussa, alisema ni vema serikali ikaharakisha kungana mkono jitihada za wananchi ili waweze kuiamini zaidi.

Alisema sehemu hiyo ya daraja imekuwa kikwazo kwa wananchi kushindwa kuzifikia huduma muhimu na kuongeza kuwa wananchi wengi wameathiriwa na mvua hizo na kaya nyingi zimekosa makazi.

Alisema serikali ya mtaa ipo karibu na wananchi hao na tayari wanaendelea kufanya tathimini ili kujua kaya zilizokumbwa na hali hiyo.

Zaidi ya sh. milioni moja zimechangwa na wananchi kwa ajili ya kukarabati miundombinu hiyo katika eneo hilo la daraja la Kinyerezi Ukonga.

No comments:

Post a Comment