Na Suleiman Abeid, Maswa
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, wazee katika Wilaya ya Maswa, mkoani Shinyanga, wamemuomba Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Bw. Augustino Mrema, kuitembelea halmashauri ili kubaini ubadhirifu mkubwa wa fedha za wananchi.
Ombi hilo limetolewa juzi na Kamati ya Baraza la Wazee wilayani humo wakati wakiwakilisha kero mbalimbali kwa wabunge wa Jimbo la Maswa Mashariki na Maswa Magharibi Bw. Sylivestar Kasulumbayi na Bw. John Shibuda wote kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Katika kikao hicho, wazee hao walieleza kusikitishwa kwao na unadhirifu wa fedha zinazokusanywa katika halmashauri, vitendo vya rushwa na kuunga mkono hoja ya madiwani wa halmashauri hiyo kumtaka Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Bw. Edward Hosea kuitembelea Wilaya hiyo.
Wazee hao wameiomba kamati hiyo, kufika mara moja wilayani humo ili kupitia hesabu za mapato na matumizi kwani halmashauri hiyo imekithiri kwa vitendo vya ubadhirifu na rushwa miongoni mwa watendaji.
Walisema baadhi ya watendaji katika halmashauri hiyo licha ya kukaa miaka mingi, wanahujumu fedha za Serikali Kuu ambazo zinatolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo pamoja na mapato ya halmashauri.
“Ubadhirifu unaofanywa na watendaji hawa, unachangia miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango hivyo kusababisha ichakae mapema baada ya kuzinduliwa.
Mmoja wa wazee hao Bw. Hamis Hassan, alisema baadhi ya watumishi katika halmashauri hiyo wanafanya jitihada mbalimbali za kukwepa uhamisho pale wanapotakiwa kuhamishwa ili waendelee kuhujumu miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema watumishi hao wameigeuza halmashauri hiyo kitega uchumi hivyo ni vyema kamati ya Bw. Mrema ikaona umuhimu wa kutembelea Wilaya hiyo kukagua mahesabu ili kuwabaini watumishi wabadhirifu.
Kwa upande wake, mbunge wa Maswa Magharibi, Bw. John Shibuda, alikubalina na mawazo ya wazee hao na kusema kuwa, wakati umefika kwa kamati hiyo kutembelea halmashauri hiyo ili kubaini madudu yanayofanywa na watendaji ambao wanakwamisha juhudi za Serikali kumaliza kero za wananchi.
LAAC kukagua mahesabu mjini Maswa
ReplyDeleteHili ni jambo jema lakini wazee hawa inatakiwa waelimishwe kwamba LAAC haikagui mahesabu bali Mkaguzi ni Ofisi ya CAG kazi ambayo nina uhakika amekwishafanya.kinachotakiwa ni wao kuelezea ubadhirifu wa makusanyo hayo umefanyika vipi kwani kinachoonekana ni majungu tu hakuna haja ya LAAC kufanya ukaguzi bali wao waeleze kwa sababu inaonekana wanajua na mambo yakiwa tofauti basi washtakiwe kwa kuharibu majina ya watumishi wa Halmashauri hiyo.
Mpanda Haki.