Na Mohamed Hamad MANYARA
MKUU wa Mkoa wa Manyara, Bw. Elaston Mbwillo, amesema tatizo la migogoro ya ardhi linatishia usalama wa maisha ya wananchi mkoani humo.
Bw. Mbwillo aliyasema hayo juzi katika Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika mjini Kibaya na kuongeza kuwa, umefika wakati wa wananchi wenyewe kutafuta njia za kumaliza na kuepuka migogoro hiyo.
Maeneo yaliyokubwa na tatizo hilo mkoani humo ni Mortangos Wilaya ya kiteto, Kirusix mjini Babati, Wilaya ya Simanjiro na Hanang ambako kuna migogoro mingi isiyokwisha.
“Nawaomba viongozi wangu kama mnataka kueleweke kwa wananchi ni vyema muwajibike kwao, huwezi kujiita kiongozi wakati kila kukicha kuna kero za wananchi, kwa nini msitatue kero zao au kuna maslahi mnayopata,” alisema.
Aliongeza kuwa, wakati mwingine kero hizi ndizo zinafanya wananchi wakose imani na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hivyo kuamua kujiunga na vyama vya upinzani na kupata nguvu ya kuisema Serikali ya chama tawala.
Aliwaagiza viongozi wa chama na Serikali kutoona aibu kutangaza mafanikio yaliyopatikana tangu Uhuru kwani Serikali ya CCM imefanya mambo mengi makubwa ili wananchi waendeleze imani yao kwa chama hicho.
“Bila kutangaza tulichokifanya kwa kipindi chote cha uhuru wanachama wetu wataendelea kutuhama, wapinzani wnatusema vibaya kuwa hakuna maendeleo tuliyoleta katika kipindi chote cha miaka 50 ya uhuru,” alisema Bw. Mbwillo.
Alimtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto Bi. Jane Mutagurwa, kuacha tabia za kukaimisha nafasi yake kwa wakuu wa Idara ili kuongeza uwajibikaji.
No comments:
Post a Comment