Na Yusuph Mussa, Kilindi
MBUNGE wa Kilindi, mkoani Tanga, Bi. Beatrice Shelukindo, amewaongoza madiwaniwa halmashauri hiyo kupinga rasimu ya Sheria Ndogo ya Afya na Usafi wa Mazingira.
Akizungumza hivi karibuni katika Kikao cha Baraza la Madiwani, Bi. Shelukindo alisema utungwaji wake haujazingatia mazingira kwa kuwataka wamiliki wa bucha za nyama waweke marumaru katika maduka yao.
Alisema sheria hiyo pia haijafafanua wazi watu wanaokataliwa kujisaidia haja ndogo ni wale waliopo miji au pamoja na wale wanaotembea porini.
“Hii sheria mliyotunga ni kandamizi, haikuangalia mazingira ya wenyeji wa maeneo haya na imekaa kwa matumizi ya Jiji la Dar es Salaam au Tanga, yaani umwambie mwenye bucha awe na kibanda cha kudumu, kiwe na maji ya bomba.
“Sheria inataka kuta za bucha zipigwe marumaru na kukataza wasikate nyama katika magogo, hivi mnazungumzia Wilaya ya Kilindi au mijini, pia hamjaweka wazi mnaposema watu wasikojoe bila kutaja maeneo gani, mijini au porini, sheria hii haitufai,” alisema.
Diwani wa Kata ya Negoro Bw. Ahmad Madoti, alisema sheria hiyo inarudisha kodi ya maendeleo kwa wananchi inaposema kila mwananchi atoe sh. 3,000 kwa mwezi ya usafi katika eneo lake ambapo kwa mwaka sh. 36,000.
“Sheria hii inawarudishia wananchi kodi ya maendeleo, hivyo tunaipinga ili ikarekebishwe, haiwezekani mwananchi atozwe tozo la sh. 3,000 kila mwezi kwa ajili ya usafi" alisema Bw. Madoti.
Mwanasheria wa halmashauri hiyo Bw. Edward Mhina, alisema sheria hiyo hata kama ingepitishwa na madiwani isingeweza kutumika kwani haikupelekwa kwa wadau (wananchi) kutoa maoni yao na kupitishwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Bi. Bibie Mnyamagola, alisema sheria hiyo bila kushirikisha mwanasheria hivyo wanairudisha ili ikafanyiwe marekebisho.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, inakataza wavulana kwa wasichana ambao hawajafikisha umri wa miaka 18kutoingia gesti, labda wanapokuwa safarini na wazazi wao.
mnapotunga sheria mzingatie mazingira na wakazi waliopo.............
ReplyDelete