10 November 2011

Watanzania watakiwa kudumisha utamaduni

Na Heri Shaaban

WATANZANIA wameshauriwa kudumisha na kuuenzi utamaduni wa asili, ili kuulinda usipotee na hata vizazi vijavyo viweze kuutambua na kuuendeleza.

Hayo yalielezwa juzi na Gloria Matola, ambaye ni mlezi wa kikundi cha vijana wa Nguvu Kazi kilichopo Kata ya Yombo Vituka Wilaya ya Temeke, Dar es salaam wakati  Mbunge wa Viti Maalumu CCM Mkoa wa Dar es salaam, Angelina Kairuki alipokitembelea kikundi hicho.


Gloria alisema ameamua  kuwakusanya vijana wenye vipaji, kutoka maeneo mbalimbali la jiji la Dar es salaam na kuwaweka  pamoja na kuunda kundi la burudani ya sanaa asilia ya Mtanznia.

"Kikundi hiki cha Nguvu Kazi, kina
vijana 30 mpaka sasa ambao waliojiunga tangu mwaka 2004. Awali kulikuwa na wanachama 10 wanawake 5 na wanaume 5," alisema.

Alisema katika kikundi hicho, wanakabiliwa na changamoto za ukosefu wa ngoma, sare za mazoezi vifaa vya ofisi kama kompyuta na ofisi ya kudumu.

Naye Mbunge Angelina, alilipongeza kundi hilo kwa kujikusanya pamoja na kutoa burudani badala kufanya ng'ono zembe na magenge ya dawa za kulevya.

Aliwataka vijana waitumie vizuri nafasi walioipata, ili taifa lisipoteze vijana wake na kujitumbukiza katika vitendo viovu.

No comments:

Post a Comment