10 November 2011

Nchimbi kuongoza kongomano Nov. 23

Na Amina Athumani

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Nchimbi ataliongoza kongamano  kubwa la michezo, linalotarajia kufanyika Novemba 23 mwaka huu.


Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Maulid Kitenge alisema mbali na Waziri ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusimamia michezo, pia viongozi wakubwa mbalimbali watashiriki kongamano hilo.

Kitenge alisema kongamamo hilo litafanyika jijini Dar es Salaam, ila bado hawajapanga litakapofanyikia na wanategemea kuwakutanisha wadau 400, kutoka sehemu mbalimbali nchini.

"Tutakuwa na wadau kutoka Wizara ya Ardhi, Afya, Maliasili na Utalii, Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambapo pia kutakuwa na wadau wengine ambao wapo katika nyanja mabalimbali za michezo," alisema  Kitenge.

Alisema kongamano hilo litakuwa na mada zisizopungua tisa, zitakazohusiana na masuala ya michezo, ambazo zitajadiliwa na kutolewa ufafanuzi.

Kitenge alisema watajadili nini tatizo la michezo ya Tanzania kutofanya vizuri katika medani ya kimataifa, kama ilivyo kwa nchi nyingine.

Ofisa huyo alisema kongamano hilo litakuwa la siku tatu, ambapo lengo lake ni kutoa fursa kwa kila mdau kuchangia na linatarajia kumalizika Novemba 25 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment