17 November 2011

Wananchi walia na uzembe wa serikali mgomo wa daladala Dar

Na Benjamin Masese

MGOMO wa mabasi madogo ya abiria maarufu kama daladala yaendayo Kigogo Mburahati Kinondoni Dar es Salaam kushinikiza barabara hiyo kutengenezwa umeingia siku ya pili huku maelfu ya wananchi wa eneo hilo wakilaani vikali serikali kushindwa kuchukua hatua kurekebisha miundo mbinu hiyo.
Mgomo huo unaoendeshwa na Umoja wa Madereva wa Mabasi ya Abiria Mkoa wa Dar es Salaam (UWAMADAR) ulioanza juzi hivyo kuwapa wakati mgumu viongozi husika wa serikali baada ya kushindwa kutimiza ahadi ya makubaliano yao ya juzi ya kutengeneza kipande kibovu cha barabara hiyo kilichosababisha magari kushindwa kupita kirahisi.

Kiini cha mgomo huo ni eneo la Landan bar kuharibika na kuwa na mashimo makubwa hivyo kukusanya maji mengi ambayo huharibu magari hayo ambapo  jumatatu jioni jumla ya magari matatu yalizimika kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kunyonya maji kwenye injini kabla ya mgomo huo kuanza siku ya Jumanne asubuhi.

Mgomo huo ulidaiwa kusitishwa kwa muda baada ya viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa Mkoa Bw. Mecky Sadiki, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Jordan Rugimbana, na viongozi wengine kutoka Mamlaka ya Udhibiti usafi wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam kukutana na UWAMADAR na kuahidi kufanya matengenezo mara moja kuanzia jana asubuhi.

Hata hivyo Majira ilipofika eneo hilo hakukuwa na shughuli yoyote ya ujenzi iliyokuwa ikifanyika hivyo kulazimika kuwatafuta viongozi wote wanaohusika licha ya Bw. Sadiki kupita eneo hilo akiwa na gari lake bila kusimama.

Katika Ofisi za Bw. Sadiki tulipokwenda kupata ufafanuzi wa chanzo cha kutotimiza ahadi zao kiongozo huyo alisema alipita eneo hilo ili kushuhudia kama ujenzi unafanyika na baada ya kuona hali hiyo aliwasiliana na Meneja wa TANROADS Dar es Salaam Bw. James Nyabakari, na kumwagiza kufanya aliwezalo kupeleka vifusi katika eneo hilo kuwaondolea wananchi kero.

Mkuu huyo wa mkoa alisema utengezaji wa barabara hiyo utafanywa bila kuathiri mipango ya mkandarasi anayetengeenza barabara hiyo kwa kiwango cha lami na kuepuka kubomoa nyumba za mwananchi waliofungua mahakamani.

Alipotafutwa kwa njia ya simu Bw. Nyabakari ili kueleza hatua alizofikia alisema wamekubaliana na mkandarasi kuanza ukarabati eneo hilo na tayari amefika eneo husika na kuanza kuondoa maji yaliyojaa barabarani.

Alisema tatizo lilipo na changamoto kubwa ni namna ya kutafuta vifusi vya kumwaga eneo hilo kwa maelezo kuwa malori yanashindwa kufuata vifusi kwa kuhofia kukwama machimboni kutokana na mvua zinazoendelea.

"Hivi sasa tunaondoa maji barabarani ili gari ziwezi kupita, suala la kujaza vifusi linatuwia vigumu kwa sababu malori hayawezi kwenda machimbo kwani yatakwama kama unavyojua mvua zinazonyesha, mkandarasi amekataa kupeleka gari huko lakini tunaendelea kutafakari jinsi ya kufanya,"alisema.

Alipotafuta Katibu wa UWAMADAR Bw. Khamis Mtumwene, kwa njia ya simu mchana alikanusha vikali taarifa za mkandarasi kufika eneo hilo bovu na kuongeza kwamba tangu asuhuhi walikuwa hapo na hakuna kilichofanyika hivyo wao wanaendelea kusubiri utekelezaji wa ahadi ya serikali.

Alisema hata kama maji yangeondolewa eneo hilo suala la ubovu uko pale pale kwa kuwa kuna mashimo makubwa yanayowavunjia vifaa mbalimbali vya magari yao na kuongeza kuwa kama ni kuondoa maji pekee hata wao wenyewe wamekuwa wakifanya hivyo pale yanapozidi na wangeendelea kufanya hivyo lakini magari yao yanazidi kuharibika huku serikali ikikaa kimya.

Kwa upande wao wananchi waliozungumza na Majira walisema hawaamini kama kweli mkoa wa Dar es Salaam una uongozi wa serikali unaowajali na kuhoji uhalali wa wao kukosa usafiri kwa madai ya ubovu wa barabara wakati kuna mkandarasi katika eneo hilo.

"Kuanzia jana (juzi) tunalazimika kutumia tex kwa sh. 15000 kwenda kazini au kuzunguka Manzese kwa nauli ya sh.1000 kutoka Kigogo mwisho, Festini au Mbuhati NHC, watu wa serikali wanapita tu magari yao makubwa, hii nchi imefika pabaya, kwa nini Magufuli asitoke uko bungeni aje ajinee mwenyewe?Alihoji Bi. Asha Ally mkazi wa Kigogo Mwisho.

Wananchi hao walisema wanaishangaa serikali kusuasua kutengeneza miundo mbinu ya kuongeza kuwa eneo hilo kama kungekuwa na viongzoi wanaowajali wananchi na kuwajibika isingefikia hatu iliyopo sasa hata kama kuna kesi mahakamani.

Hii ni mara ya pili kwa daladala kugoma kutokana na eneo hilo kutokana na ubovu wa barabara. Barabra hiyo inayounganisha Kariakoo-Msimbazi, njia panda ya Kigogo hadi Ubungo maziwa unajengwa kwa kiwango cha lami huku baadhi ya maeneo yakichwa kwa madai ya kesi zilizofunguliowa na wananchi.

1 comment:

  1. Hivi kwanini msitumie matrekta kuchota hivyo vifusi na kisha kwenda kujaza kwenye malori?.Unaposema malori yanakwama,unamaana ya kuwa hayo malori ndiyo yanayochimba hivyo vifusi?Viongozi wacheni kuongea uongo ambao hauna kichwa wala miguu.

    ReplyDelete