Na Godfrey Ismaely Dodoma
WAZIRI wa Katiba na Sheria Bi. Celina Kombani, amewahimiza wananchi
kushiriki katika maadhimisho ya miaka 50 ya wizara hiyo yatakayoanza leo ili waweze kuwasilisha maoni yao na kero zinazowakabili kwa upande wa
sheria sambamba na huduma za usajili wa vizazi.
Wito huo aliutoa jana mjini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya uziduzi wa maadhimisho hayo yatakayofanyiwa na Jaji Kiongozi Bw. Fakihi Jundu, katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
"Napenda kuwataarifu wananchi kuwa kesho (leo) Alhamisi Novemba 17 hadi
jamapili Novemba 20, 2011 sekta ya sheria na katiba chini ya utaratibu wa
wizara ya Katiba na Sheria itakuwa inaadhimisha miaka 50 ya Uhuru
tulioupata mwaka 1961.
Maadhimisho haya yatazinduliwa na Jaji Kiongozi Mheshimiwa Fakihi Jundu, katika maadhimisho haya maofisa mbalimbali kutoka katika sekta hii watafanya shughuli mbalimbali zinazolenga kuwaelimisha wananchi kuhusu historia, mafanikio, changamoto na mipango inayolenga kuboresha sekta hii," alisema Bi.Kombani.
Alisema katika maadhimisho hayo taasisi mbalimbali zitashiriki zikiwemo za
serikali na zile zisizo za kiserikali ambazo ujishughulisha na masuala ya
sheria nchini.
"Katika siku hizo nne huduma za msingi ambazo kila mwananchi atapatiwa ni
pamoja na elimu, huduma za usajili wa vizazi chini ya wakala wa
Usajili,Ufilisi, na Udhamini (RITA), msaada wa kisheria, kupokea malalamiko
kuhusu vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu sambamba na burudani
mbalimbali," alisema Bi. Kombani.
Waziri huyo alisema licha ya changamoto mbalimbali ambazo Taifa limekuwa
likipitia ndani ya miaka 50 ya Uhuru kuna hatua kubwa ambazo zimepigwa
katika sekta ya sheria.
"Kwa mfano tumeongeza idadi ya watumishi wa ngazi zote kwa kiasi kikubwa
kwa kuwa mwaka 1961 tulikuwa na majaji saba tu, tena wote wageni, leo tuna majaji zaidi ya 70 na wote ni watanzania ikiwemo kupiga hatua ya kuongeza Masjala za mahakama Kuu katika mikoa yetu kutoka tatu hadi kufikia masjala 13.
Ni fursa ya pekee kwa wananchi wote waishio Dar es salaam na mikoa jirani kutembelea Mnazi mmoja ikiwa ni pamoja na kufuatilia vyombo vya habari mara kwa mara," alisema Bi. Kombani.
No comments:
Post a Comment