Na Suleiman Abeid, Shinyanga
SAKATA la wafanyakazi wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi wilayani Kahama Mkoani
Shinyanga kufungua jalada la kutukanwa na mmoja wa waajiri wa mgodi huo
polisi limechukua sura mpya baada walihusika kufungua jalada hilo kuanza kufukuzwa kazi.
Wakati uongozi wa mgodi huo ukianza kuwafukuza kazi wafanyakazi hao, Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga nalo limeendelea kupiga danadana na kushindwa kumfikisha mahakamani mtuhumiwa wa matusi kwa wafanyakazi aliyedaiwa kuwaita ‘mbwa wadogo’ kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi na Viwanda nchini (TAMICO) Mkoa wa Shinyanga, Bw. Mwita Bhoke, kitendo cha uongozi wa mgodi huo kuamua kuwafukuza kazi wafanyakazi hao kwa sasa kinalenga kupoteza ushahidi wa kutukanwa kwao pale mtuhumiwa atakapofikishwa mahakamani.
Alisema mara baada ya wafanyakazi kufungua jalada la kutukanwa polisi na mmoja wa wasimamizi wa mgodi huo (jina tunalo) mwajiri ameanza kuwaundia wafanyakazi tuhuma za uongo kwa lengo la kufanikisha adhima yake ya kuwafukuza kazi huku wengine akiwasimamisha kinyume cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini namba 6 ya mwaka 2004.
Alisema TAMICO imebaini kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu zilizotumika katika kuwasimamisha kazi wafanyakazi hao na wengine kufukuzwa utaratibu ambao unamtaka mwajiri kabla ya kuchukua hatua hizo mfanyakazi ana haki ya kufanya mazungumzo na Tawi la TAMICO mgodini kama mkataba unavyoelekeza.
Alisema mpaka sasa tayari wafanyakazi 16 kati ya 40 waliofungua jalada hilo la kutukanwa wamesimamishwa kazi huku watatu wakifukuzwa kabisa hali ambayo inatia wasiwasi kuwa huenda viongozi wa mgodi huo hawaheshimu sheria zilizopo nchini za vyama vya wafanyakazi.
Alisema wafanyakazi waliosimamishwa pamoja na wale waliofukuzwa wametuhumiwa kwa makosa ya kusingiziwa ambapo uongozi wa mgodi ulidai walikula njama za kutaka kuhujumu na kuharibu baadhi ya mali na mitambo ya mgodi huo kwa kuweka soda na chumvi katika mitambo iliyoko katika maeneo yao ya kazi madai ambayo hayana ukweli.
Kwa upande wake katibu wa TAMICO Wilaya ya Kahama, Bw. Patarnus Rwechungura, alisema wakati chama chake kikijipanga kufanya vikao vya pamoja kwa lengo la kujadili mgogoro uliojitokeza uongozi wa mgodi huo umekuwa hautoi ushirikiano wowote.
Alisema uongozi wa mgodi huo hautoi majibu ya barua zote wanazopelekewa zikiomba kufanyika vikao kati ya menejimenti na viongozi wa TAMICO jambo ambalo ni dharau kubwa kwa wafanyakazi,chama na watanzania kwa ujumla.
Bw. Rwechungura alisema kutokana na kitendo hicho cha kukosa ushirikiano, chama chake kinajipanga kufungua kesi katika Tume ya usuluhishi na uamuzi (CMA) kwa vile hata masuala ambayo wamekuwa wakikubaliana na mwajiri utekelezaji wake upande wa mwajiri umekuwa ni wa kusuasua.
Aliyekuwa Katibu wa Tawi la TAMICO mgodini hapo Bw. Johnson Mbando, ambaye ni miongoni mwa wafanyakazi waliosimamishwa kazi alisema kitendo walichofanyiwa na uongozi wa mgodi huo ni cha unyanyasaji mkubwa na kwamba amelilaumu Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga kwa kitendo cha kumkingia kifua mtuhumiwa.
Bw. Mbando alisema pamoja na wafanyakazi 40 kufungua jalada polisi Oktoba 9, mwaka huu, lakini mpaka sasa polisi hawajamchukulia hatua zozote mtuhumiwa aliyewatukana ambaye hata hivyo kwa hivi sasa ameishaondoka nchini akidaiwa kuchukua likizo fupi na sasa yuko nyumbani kwao nchini Marekani.
Alisema kutokana na polisi kushindwa kumchukulia hatua mtuhumiwa huyo huku
wafanyakazi waliofungua kesi wakifukuzwa kazi, hivi sasa wanatafuta msaada wa wanasheria na watetezi wa haki za binadamu ili waweze kuwasaidia kufungua kesi moja kwa moja mahakamani kupinga kitendo cha wao kutukanwa na wageni huku polisi wakiona ni sawa kwa kuwa ni wawekezaji.
Hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga lilikiri wafanyakazi hao kufungua jalada la kutukanwa na mmoja wa waajiri wa mgodi huo wa Buzwagi na kudai kuwa lilishindwa kuchukua hatua za kumkamata mtuhumiwa mpaka litakapokamilisha uchunguzi kubaini ukweli wa madai hayo ya wafanyakazi.
Kauli ya jeshi hiyo iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Bw. Diwani Athumani, ilipingwa vikali na wafanyakazi hao na kuonesha wasiwasi wao juu ya majibu hayo.
Wafanyakazi hao walidai uzoefu unaonesha kwamba mtu anapofungua kesi kama hiyo mtuhumiwa hukamatwa kwanza ndipo hatua za uchunguzi hufuata baadaye na kuhoji ni lini jeshi la polisi kubadili utaratibu huo ni kwa watu wanyonge pekee.
Polisi wa Maghamba. Ni ajabu kuwa mgeni anatukana wenyeji anachekelewa tu. Kwa vitendo hivi vya polidi ndio maana mzungu anawaita mbwa wadogo. Ni dhahiri kawatukana polisi hao pia kuwa ni mbwa wadogo.
ReplyDelete