18 November 2011

Jaji Kiongozi ataja mafanikio sekta ya sheria

Na Salim Nyomolelo

WANANCHI wameombwa kujitokeza kwa wingi kupata huduma mbalimbali za kisheria na maelezo ya kina kuhusu maendeleo ya sekta hiyo katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam bila malipo.


Pia wameshauriwa kuhudhuria viwanja hivyo ili kuona na kupata msaada wa Sheria na Katiba, vyeti vya ndoa na talaka pamoja na vyeti vya vizazi na vifo ambapo huduma hiyo inatolewa pia bila ya malipo yoyote.

Akizungumza katika ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 50 wa uhuru wa Tanzania Bara kwa upande wa Wizara ya Katiba na Sheria jana, Jaji Kiongozi Bw. Fakih Jundu, alisema wananchi watakaofika katika maeneo hayo wataweza kupatiwa msaada wa sheria pamoja na kupata fursa ya kujua haki za binadamu.

Alisema pia katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru Tanzania Bara sekta ya sheria kwa ujumla iliweza kupiga hatua mbalimbali ikiwemo ongezeko la majaji.

"Mwaka 1961 tulikuwa na majaji saba na mawakili wa serikali 10 wakati hii leo tuna majaji 57 na mawakili wa serikali zaidi ya 300," alisema.

Alisema wataendelea kupanua mtandao wa huduma zao kwa kuongeza watumishi pamoja na kushirikiana na wadau wengine ili kuendelea kujenga na kufungua mahakama za ngazi zote ikiwemo ofisi ya mwanasheria mkuu katika mikoa yote.

"Tunapenda kuboresha mfumo wetu wa mashtaka na upelelezi ili kuongeza ufanisi katika usikilizaji wa mashauli,"alisema.

Kwa upande wa baadhi ya washiriki waliofika katika viwanja hivyo jana walisema hawaoni umuhimu wa maadhimisho hayo kwa maelezo kuwa watu wengi wamekuwa wakitendewa vitendo viovu lakini mamlaka hiyo ina kaa kimya.

No comments:

Post a Comment