11 November 2011

Tutajadili maadili na uadilifu nchini-Butiku

Na Rehema Maigala

TAASISI ya Mwalimu Nyerere imeandaa mdahalo wa siku mbili kujadili na kuzingatia nafasi na umuhimu wa Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika maisha ya watanzania.


Akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Bw. Joseph Butiku, alitaja lengo kuu la mdahalo huo kuwa ni kusisitiza misingi mikuu ya Katiba na maadili ya uadilifu.

"Mdahalo wetu utazungumzia jinsi ya kujikumbusha maana na misingi yetu ya kitaifa ambayo imechangia utambulisho wetu kama Watanzania taifa lenye umoja, amani, upendo na udugu ambayo hayo yote yapo katika katiba yetu," alisema Bw. Butiku.

Alisema kupitia mdahalo huo watanzania watatafakari wapi tulipotoka, tulipo sasa katika maisha ya Utaifa, nini cha kufanya ili kuimarisha maadili katika Taifa kwa kuzingatia ukweli kwamba katiba ndiyo msingi wa maadili ya watanzania au Taifa lolote kutoa maoni na mapendekezo.

Alisema pia watanzania watatafakari kuhusu maeneo na misingi ya kuzingatia katika kujadili na kuandaa rasimu ya mabadiliko ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo marekebisho ya Katiba ya Tanzania Visiwani.

Alisema mada kuu katika mdahalo huo utakuwa ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania huku mada ya pili ikiwa msingi wa maadili ya Taifa.

Bw. Butiku alimtaja anayetarajiwa kutoa mada katika mdahalo huo kuwa ni Profesa Palamagamba Kabudi, kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mdahalo pia utawashirikisha wanasheria mbalimbali.

No comments:

Post a Comment