11 November 2011

Mbowe afikishwa kortini Arusha

Akabiliwa na makosa mawili

Na Queen Lema, Arusha

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Freeman Mbowe, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha akikabiliwa na makosa mawili.


Akisomewa mashitaka yanayomkabili mahakamani hapo jana, Mwendesha Mashitaka wa Serikali Bw. Haruna Matagani, mbele ya Hakimu wa Hahakama hiyo Bi. Devotha Kamuzora, alidai Bw. Mbowe alitenda makosa hayo kwenye mkutano wa hadhara.

Katika kosa la kwanza Bw. Mbowe alidaiwa kuwa ni miongoni mwa watu ambao waliongoza mkesha uliofanyika baada ya muda wa mkutano kumalizika jambo ambalo ni kinyume cha sheria na taratibu za Jeshi la Polisi.

Katika kosa la pili Bw. Mbowe anakabiliwa na shtaka la kukataa kutii amri halali ya polisi ya kuwataka kutawanyika kwa sababu za kiusalama.

"Jeshi la polisi liliwataka wafuasi watawanyike baada ya kumalizika kwa mkutano ambao ulikuwa na kibali halali, lakini haikuwa hivyo badala yake waliendelea na mkutano," alidai mwendesha mashitaka na kuongeza kuwa Jeshi la Polisi lilizidi kuwasihi watawanyike lakini walikiuuka amri.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Bw. Mbowe aliyakana yote. Kesi hiyo iliahirishwa hadi November 22, mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Mwanasiasa huyo anayetetewa na wakili Bw. Methody Kimomogoro aliachiwa baada ya kutekeleza masharti ya dhamana.

Bw. Mbowe ni mshtakiwa wa 28 kushitakiwa kutokana na makosa wanayodaiwa kuyafanya kwa kukiuka masharti ya polisi na badala yake kuendesha mkesha kwenye Viwanja vya NMC kwa lengo la kushinikiza Mbunge wa Arusha Mjini Bw. Godbless Lema, kuachiwa kwa dhamana baada ya kukataa haki hiyo awali.

Wengine waliofikishwa mahakamani hapo ni Mbunge wa Singida Mashariki, Bw. Tindu Lissu na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibroad Slaa. Tofauti na washitakiwa wengine, Bw. Slaa anakabiliwa na shtaka la uchochezi.

Katika hatua nyingine mji wa Arusha umeonekana kuwa shwari zaidi baada ya kusitishwa kwa maandamano ambayo yalikuwa yamepangwa na CHADEMA jana kuzuiwa na polisi kwa sababu za kiusalama.

Awali Mbunge Lema alikataa dhamana kwa kile alichodai kuwa ni kwenda mahabusu kutetea haki na kwamba hilo ni eneo zuri linalofaa kwa kupigania haki hivyo mahakama kuahitisha kesi yake hadi Novemba 14 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment