Na Victor Mkumbo
KIKOSI cha timu ya taifa ya pool, kimeondoka jana kwenda nchini Malawi kushiriki katika mashindano ya All African Cup, yanayotarajiwa kuanza Novemba 22 hadi Novemba 26 mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Meneja wa bia ya Safari Lager ambao ndiyo wadhamini wa timu hiyo, Oscar Shelukindo alisema kikosi hicho kitarejea na ushindi kutokana kujiandaa vyema.
Alisema timu hiyo, ilikaa kambini kwa wiki moja kujiwinda na mashindano hayo, ambayo yanatarajia kushirikisha nchi 14 kutoka Afrika.
Shelukindo alizitaja nchi zitakazoshiriki kuwa ni wenyeji Malawi, Zimbabwe, Cameroon, Zambia, Uganda, Swaziland, Reunion FBB, Reunion Arabas, Nigeria, Msumbiji, Morocco, Lesotho na Tanzania.
“Timu inaondoka lakini safarini itapita katika mikoa ya Morogoro, Iringa na Mbeya kwa ajili ya kucheza michezo ya kirafiki," alisema.
Timu hiyo ilikabidhiwa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi bendera, Malinzi aliwataka wachezaji wa timu hiyo kurudi na ushindi.
“Timu hii ndiyo imebeba dhamana ya Watanzania zaidi ya milioni 40, hivyo tunatarajia itapeperusha vyema bendera yetu na kurudi na ushindi,” alisema.
Naye Kocha Mkuu wa timu hiyo, Denis Lungu aliwataja wachezaji waliokwenda Malawi kuwa ni Omary Akida, Felix Athanas, Godfrey Mhando, Mohamed Idd, Charles Venance, Anthony Thomas, Shamis Nassor na Abdallah Hussein
No comments:
Post a Comment