Na Zahoro Mlanzi
TIMU za JKT Oljoro na Simba, zitapambana leo asubuhi kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam katika robo fainali ya michuano ya Uhai Cup.
Wakati timu hizo zikimenyama huko, kwenye Uwanja wa Chamazi, muda huo huo kutakuwa na mechi kati ya JKT Ruvu Stars na Toto African.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mechi nyingine zitachezwa jioni ambapo Serengeti Boyz (timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17) itaumana na Villa Squad.
Alisema mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Karume na kule Chamazi Moro United itaumana na Azam.
Alisema nusu fainali itachezwa Novemba 23, mwaka huu Uwanja wa Karume ambapo mechi ya kwanza itakuwa asubuhi na nyingine jioni huku fainali itapigwa Novemba 25 saa 9 alasiri ikitanguliwa na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu itakayoanza asubuhi.
Bingwa wa michuano hiyo atapata sh. milioni 1.5, mshindi wa pili sh. milioni moja wakati wa tatu atapata sh. 500,000. Mbali ya fedha hizo, bingwa atapata medali za dhahabu, makamu bingwa medali za fedha na mshindi wa tatu medali za shaba.
Mchezaji bora sh. 400,000, mfungaji bora (sh. 300,000), kipa bora (sh. 300,000) na timu yenye nidhamu sh. 300,000.
No comments:
Post a Comment