02 November 2011

Shibuda aionya CCM

Na Suleiman Abeid, Maswa


*Amtahadharisha JK kuwa makini na wasaidizi wake
*Asema wakuu wa mikoa, wilaya wameshindwa kazi
*Asisitiza ndani ya CCM hakuna sikio linalosikia la mkuu
MBUNGE wa Maswa Magharibi, mkoani Shinyanga, Bw. John Shibuda (CHADEMA), amemtahadharisha Rais Jakaya Kikwete kutowaamini sana baadhi ya watendaji wake hasa viongozi waliopo serikalini kwani ndio waliochangia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kipoteze mwelekeo na mvuto kwa Watanzania.

Bw. Shibuda aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Baraza la Wazee wilayani humo.

Alisema baadhi ya watendaji ndani ya serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa na Wilaya, wameshindwa kuwatumikia wananchi kikamilifu na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili hali iliyochangia jamii kubwa kukichukia chama hicho.

Aliongeza kuwa, Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Majiji, Manispaa na ambao wanateuliwa na rais, wameshindwa kutoa ushirikiano kwa wananchi kama walivyokula kiapo wakati wa kuapishwa hali iliyochangia wananchi kukosa viongozi wa kuwasaidia na kutatua kero zao.

“Baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali hawajui mipaka ya kazi zao licha ya kuwa na madaraka makubwa, badala yake wamejigeuza miungu watu na mamangimeza hivyo kusababisha kero kwa wananchi kwa sababu ya kwenda kinyume na dhana nzima ya utawala bora,” alisema Bw. Shibuda.

Kutokana na hali hiyo, Bw. Shibuda ambaye kabla ya kuhamia CHADEMA alikuwa mmoja wa makada wa CCM, alisema ni vyema Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), ikahamishiwa katika Ofisi ya Rais, Utawala Bora kwa kile alichodai Ofisi ya Waziri Mkuu, imeshindwa kuisimamia vizuri Wizara hiyo.

Alisema vitendo vingi vya wizi na ubadhirifu wa fedha za wananchi katika Halmashauri za Wilaya, vinasababishwa na usimamizi mbaya hivyo ni wazi kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu imeshindwa kazi.

Katika hatua nyingine, Bw. Shibuda alizunguzia makundi yaliyopo ndani ya CCM na kusema kuwa, hali hiyo imechangiwa na Rais mwenyewe kushindwa kuwakemea viongozi na watendaji wa chama ambao wanakwenda kinyume na maadili ya kazi zao.

Alisema mpasuko uliopo ndani ya CCM kwa sasa, unasababishwa na makundi yasiyovumiliana na kusameheana badala yake yamekuwa yakihujumiana na kuwekeana visasi visivyo na kikomo jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya chama.

“Hata katika vitabu vya dini suala la kuwekeana visasi limekemewa sana, Rais Kikwete asipokuwa makini ipo hatari ya CCM kuifia mikononi mwake kitu ambacho nisingependa kitokee kwani kama chama hiki kitakufa, CHADEMA watakosa chama cha kupambana nacho katika ulingo wa siasa.

“Napenda CCM iendelee kuwepo, ili sisi CHADEMA tuishinde na tuwe vyama viwili shupavu kama ilivyo katika nchi za Magharibi, Marekani na Uingereza, maana pakiwepo na ushindani wa kweli, maendeleo ya Watanzania yataharakishwa ndani ya demokrasia ya kweli,” alisema Bw. Shibuda.

Aliongeza kuwa, hivi sasa ndani ya CCM hakuna sikio linaloweza kusikia la mkuu, kila mtu anakwenda kivyake ndiyo chanzo kikubwa cha makundi hata kusababisha Rais Kikwete na chama chake ambacho ni kikongwe kipoteze umaarufu.

Katika kikao hicho, Bw. Shibuda ambaye aliongozana na Mbunge wa Maswa Mashariki Bw. Sylivestar Kasulumbai (CHADEMA), walikuwa wakipokea kero mbalimbali kutoka kwa wajumbe wa kamati hiyo bila kujali itikadi za vyama vyao.

Wazee hao walisema, kilio cha wananchi jimboni humo ni ongezeko la vitendo vya rushwa, ufisadi, hujuma na ubadhirifu katika miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo waliwaomba wabunge hao, kuhakikisha kero hizo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

2 comments:

  1. Wee Buda acha kuganga njaa! Kama wewe ni CHADEMA ya CCM yanakuwasha nini? Tunajua unajikomba upewe U Dc au RC! Mijitu kaa nyie ndio mmefikisha nchi hapa ilipo! Akili ziro kazi kubwabwaja eti ndio siasa! Kachunge ng'ombe au kajiunge na kikundi cha ugobogobo!

    ReplyDelete
  2. tokaaaaaaaaaaapa unataka ccm iwepo umetoka kwa nini??unatamani kurudi unaona haya wewe.....

    ReplyDelete