Na Daud Magesa, Mwanza
*Vijana UVCCM waaswa kutokubali kutumika
*Kada atahadharisha urais kujadiliwa kikanda
MJUMBE wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), mkoani Kilimanjaro, Bw. Paul Makonda, amewataka vijana nchini kutokubali kutumika ili wasiigawe nchi kwa maslahi ya watu wachache wanaotaka kuwania urais katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Bw. Makonda aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mwanza na kuongeza kuwa, viongozi jasiri ambao wanaipenda Tanzania, wanapaswa kusimama kidete na kukemea hali hiyo ili taifa lisiingie katika migogoro.
Alisema mijadala inayopamba moto ikihusisha makundi mawili ya vijana katika mikoa ya Arusha na Pwani juu ya rais ajaye atoke wapi, haina tija kwa sasa na ikiachwa iendelee, itahatarisha
amani na mshikamno uliodumu kwa muda mrefu.
“Ni vyema tukumbuke urais ni nafasi kubwa inayohusu hatma ya Taifa letu hivyo tukiacha mijadala hii iendelee ni kuhatarisha amani na mshikamano wetu, tukumbuke maneno ya wenye hekima kuwa “Waovu hustawi pale wema wanaponyamaza kimya” ndiyo maana nimeamua kulisema hili,” alisema Bw. Makonda.
Aliongeza kuwa, rais ajaye ni hoja inayoonekana kupewa kipaumbele wakati nchi inakabiliwa na matatizo mengi hususan ugumu wa maisha ya Watanzania na vijana kukosa ajira za uhakika.
“Hivi sasa nchi inakabiliwa na matatizo mengi, Watanzania wanapoamka asubuhi hajui watakula nini, vijana wa Pwani hawataki rais atoke Kaskazini, tukiingia kwenye ukanda kujadili urais, kila kanda itaibuka na sababu ukanda au udini hali ambayo itatugawa, tusielekee huko,” alisema.
Bw. Makonda aliongeza kuwa, kama nafasi ya urais itajadiliwa kikanda, kila kanda itaibuka na kutaka kutoa rais wake hivyo kusababisha mgawanyiko na mpasuko mkubwa.
“Mijadala hii ikiendelea kushika kasi, hii ni dalili ya hatari kwa umoja wetu ndani ya chama na nchi yenyewe, kwani nini tujadili rais wa 2015 wakati rais wetu yupo madarakani tena ana mwaka mmoja tu,” alisema.
Alisema migawanyiko hiyo ya kikanda kama itaachwa bila kushughulikiwa mapema, italeta mpasuko mkubwa katika nchi kwa sababu watu watasahau dini zao, vyama vyao na makabila yao badala yake wataanza kutukuza asili yao.
Bw. Makonda alisema, hivi karibuni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Bw. Steven Wassira alinukuliwa akizungumzia sifa za kumpata urais ndani ya CCM kuwa ni yule atakayeweka kipaumbele cha ajira kwa vijana.
Alisema kauli ya kiongozi huyo ni msimamo wa Serikali na kuongeza kuwa ni vyema msimamo huo ukaangaliwa upya kwani hauna tija kwa Taifa na vijana kwa ujumla.
“Msimamo huu hauwezi kuleta ajira kwa vijana wala kurudisha matumani kwa wanyonge wanaoteseka na njaa pamoja na kero nyingine, umefika wakati wa Serikali kuona umuhimu wa kuchochea mijadala yenye manufaa kuwa vijana ili wajue wananufaikeje na uwekezaji, mabilioni ya Rais Kikwete yamewanufaishaje, vijana Vyuo Vikuu watasaidiwaje na Serikali ili wapate mikopo na jinsi watakavyonufaika na soko la pamoja,” alisema.
No comments:
Post a Comment