Na Yusuph Mussa, Handeni
BAADHI ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, wamesema mauaji ya wakulima na wafugaji yanayotokea katika baadhi ya Wilaya nchini, huenda yakatokea wilayani humo kutokana na uvamizi unaofanywa na wafugaji wanaotoka mikoa ya Arusha na Manyara.
Diwani wa Kata ya Kwamatuku Bw. Mustapha Beleko, aliyasema hayo juzi katika Kikao cha Baraza la Madiwani na kuongeza kuwa, katika kata yake wafugaji wamevamia maeneo mbalimbali na kutishia uvunjifu wa amani hivyo wamepanga kuwatimua.
“Wafugaji wa Kimang'ati wanakuja na mifugo na kukata miguu ng'ombe wa wenyeji, jambo hilo linaweza kuvunja amani, tumeanza operesheni ya kuwaondoa baada ya kufikia uamuzi huu katika Kikao cha Maendeleo ya Kata (WDC).
“Kama hawa wafugaji watakataa kuondoka, tunataka kujua halmashauri utatusaidiaje maana tumechoka kuvamiwa na wafugaji wanaotoka mikoa ya Arusha na Manyara, wamekuwa wanaingiza mifugo yao kiholela,” alisema Bw. Beleko.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Bw. Hassan Mwachibuzi, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, alisema kama kutatokea kutoelewana au kukataa kuondoka, watoe taarifa wilayani.
“Kama watakataa pelekeni taarifa kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, hawawezi kukaa kwa nguvu wakati sisi hatuna eneo la kuwaweka wafugaji wageni katika Wilaya yetu, hofu yangu siju kama mtaweza kuwatoa maana wanakuja na fedha nyingi,” alisema Bw. Mwachibuzi.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Bw. Ramadhan Diliwa, aliwataka watumishi wa halmashauri hiyo kukaa chonjo kwani hivi sasa madiwani watafuatilia utendaji wao na kama watabaini uzembe wowote watachukuliwa hatua.
No comments:
Post a Comment