09 November 2011

Rais Barcelona ataka timu 16 Hispania

ZURICH, Uswisi

RAIS wa Barcelona, Sandro Rosell anataka timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Soka Hispania, kupunguzwa kutoka 20 hadi 16.
Mkuu wa Klabu hiyo ya Catalan, alisema soka la Hispania linapia katika kipindi kigumu na amependekeza kupunguzwa timu hadi 18 kwa awamu ya kwanza, kisha hadi 16 ili kurudisha ushindani.

Rosell alisema timu 20 zinazoshindana sasa katika La Liga ni Barcelona, Real Madrid, Athletic Bilbao na Osasuna pekee ambazo zina uwezo kiuchumi.

"Timu nyingine 16 ziko katika hali mbaya na siaamini kama zinaweza kupata ahueni," alisema katika mkutano uliofanyika Zurich.

"Pengine mwakani zitakuwa katika daraja la pili au la tatu, au pengine kupotea kwa pamoja."

Rais huyo wa Barcelona, alielezea mashaka kuhusu klabu za Hispania kununuliwa na wawekezaji wa nje, kama ilivyokuwa kwa Klabu za Malaga na Racing Santander.

"Swali langu ni wapi tunakwenda na kitu gani kitatokea wakati klabu hizi zinaweza kutokuwa na rasilimali," alisema.

"Wanakuja Hispania na sipendezewi na hilo, lakini hilo linatokea."

Rais huyo mwenye umri wa miaka 47, pia alielezea kuhusu mgawanyo wa mapato yanayotokana na matangazo ya televisheni kwa klabu za Hiapania na kutoa mfano wa ligi nyingine za Ulaya.

"Ligi ya Hispania ni pekee, ambayo haki za televisheni zinafanywa kwa makubaliano na watu binafsi na katika miaka minne au mitano, tutatakiwa kuwa na mgawanyo kama ilivyo kwa Serie A au Ligi Kuu," Rosell aliongeza.

No comments:

Post a Comment