11 November 2011

Poulsen ajadiliwa bungeni

Na Mwali Ibrahim

NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fenella Mukangara, jana ameshindwa kuweka sawa swali la Mbunge wa Jimbo la Dimani, Abdallah Sharia ambaye alitaka kujua ni kwanini Kocha Mkuu wa timu ya taifa (Taifa Stars), Jan Paulsen anayegharamiwa na Serikali kuifundisha na timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars).

Akijibu swali hilo katika kikao cha tano cha Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kinachoendelea mjini Dodoma, Fenella alishindwa kuliweka sawa swali hilo na badala yake akasema kwamba kocha huyo, anatakiwa kupewa ushirikiano kwa kuwa anaifunza Taifa Stars, ambayo ina wachezaji wa pande zote Bara na Zanzibar.

Kocha huyo hivi sasa yupo nchini Chad na Taifa Stars, ambayo leo itacheza na nchi hiyo katika ya kwanza ya mchujo kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014.

"Lazima tuungane na kocha, ili kuweza kuongeza mshikamano wetu kwani timu yetu ya taifa, ina wachezaji wa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar," alisema Fenella.

Hata hivyo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), humpa jukumu kocha huyo wa Taifa Stars kuifunza Kili Stars, ambayo hushiriki michuano ya Chalenji ambayo inaandaliwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ambayo timu ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) nayo hushiriki kwa kuwa ni mwanachama wa baraza hilo.

TFF pia imewahi kumtumia Kocha aliyeoondoka, Mbrazil Marcio Maximo kuifunza Kilimanjaro Stars katika michuano ya Chalenji. Maximo naye alikuwa akigharamiwa na Serikali.

Akizungumzia suala la Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA), kutotambulika na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Waziri huyo alisema suala hilo ni uamuzi wa FIFA, ambayo inasheria zake hivyo wao hawawezi kuliongelea.

Alisema, walishaanza kulishughulikia suala hilo wakishirikiana na Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF), ili ZFA kupata uanachama FIFA, lakini alipokea barua Julai mwaka huu kutoka FIFA ikionesha ZFA haiweze kupata uanachama kwa kuwa ipo ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Waziri Fennela alisema, lakini FIFA iliahidi kutoa misaada kwa ZFA kupitia TFF, ambayo ndiyo inatambulika na shirikisho hilo.

"Barua hiyo ninayo, lakini tutaendelea kufuatlia ili pindi FIFA watakapofanya mabadiliko ya katiba iweza kuiingiza ZFA kama mwanachama na kuweza kutambulika kama ilivyo kwa nchi za China na Honga Kong," alisema.

No comments:

Post a Comment