11 November 2011

Papic 'ateta' na viongozi Yanga

Na Zahoro Mlanzi

KOCHA Mkuu wa Yanga Kostadin Papic, jana amekutana na Kamati ya Usajili ya timu hiyo kuteta nayo kuhusu usajili wa dirisha dogo ulioanza Novemba Mosi, mwaka huu.

Mbali na hilo, kocha huyo amepanga kutoondoka nchini kipindi hiki cha mapumziko, akiwa na lengo la kuandaa mazingira ya kutetea ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara.


Kwa mujibu wa habari za uhakika zilizopatikana kwa mmoja wa viongozi wa Yanga Dar es Salaam jana zilieleza kwamba, Papic alikutana na kamati hiyo kuieleza kila kitu kuhusu mzunguko unaokuja.

"Wachezaji wapo likizo, lakini mikakati ya usajili inaendelea japo kimya kimya, Papic leo (jana) jioni anatarajia kukutana na Kamati ya Usajili kujadili mapendekezo aliyoyatoa," alisema mtoa habari huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

Alisema kikao hicho kitajadili wachezaji ambao Papic, amependekeza kuwaacha pamoja na wale wapya anaotarajia kamati hiyo itawasajili.

Kiongozi huyo alisema, Papic katika ripoti yake kwa Kamati ya Utendaji aliomba nafasi za ulinzi, kiungo na ushambuliaji ziongezewe nguvu kwani zinaonekana hazina ushindani.

Alisema mara baada ya kikao hicho, ambacho kilitarajia kutoa majumuisho ya mwisho yatakayopelekwa katika Kamati ya Utendaji kwa ajili ya kuthibitishwa, ndicho kitakachotoa picha halisi ya usajili wa Yanga.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Ahmed Seif kupitia simu yake ya kiganjani hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.

No comments:

Post a Comment