Na Mwandishi Wetu
KOCHA Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic ameridhia kumrudisha kundini aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Athuman Idd 'Chuji' kwa ajili ya mashindano mbalimbali.
Chuji kabla ya kurudi Jangwani, aliichezea Simba katika michuano ya Kombe la Kagame, lakini timu ilivunja naye mkataba kinyemela kabla ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kuingilia kati.
Baada ya TFF kuingilia suala hilo na kuitaka Simba, imtambue kama mchezaji wao halali, timu hiyo iliamua kumpeleka kwa mkopo Villa Squad lakini haikuichezea timu hiyo kutokana na muda wa usajili kupita.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana Dar es Salaam jana, kutoka kwa kiongozi mmoja wa Yanga alisema kwamba juzi walikuwa na kikao kizito cha Kamati ya Utendaji, kocha na Kamati ya Usajili ambapo walijadiliana kuhusu mzunguko unaokuja na kufikia muafaka.
"Tulijadiliana mambo mengi lakini kubwa ni kwamba Papic, ambaye alikuwa akisubiriwa kwa hamu kuamua kama Chuji anaweza kuichezea Yanga, angekubali hivyo jitihada zinaendelea na wiki hii kila kitu kitakamilika," alisema kiongozi huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe.
Alisema Papic, amekubali na amesema Chuji ataisaidia timu hiyo, licha ya kwamba ana matatizo yake lakini atakutana naye kwanza waweke mambo sawa.
Mbali na hilo, pia kikao hicho kilizungumzia suala la mchezaji Haruna Niyonzima, ambaye vyombo mbalimbali vya habari vinaripoti kwamba anatakiwa na Simba, ambapo kikao hicho kiliamua kitamtumia mkataba mpya huko alipo kwa ajili ya kuzima ndoto hizo.
Alisema pia wachezaji wapya wanaotakiwa na Papic, wameshajulikana pamoja na wale atakaowaacha, lakini yote hayo yatawekwa wazi siku zijazo.
No comments:
Post a Comment